Mwalimu Mkuu wa idara ya Kiswahili Idara ya Kiswahili kwa Wageni Bi. Shani Khalfan ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Withwoth cha Marekani kwa kuendelea kuichagua SUZA kupokea wanafunzi wake kwa ajili ya kuwasomesha lugha ya Kiswahili.
Alisema huduma hiyo wamekuwa wakiitoa kwa muda wa miaka 10 bila kusita na ana matumaini kuwa wataendelea kuwa pamoja katika kuikuza lugha ya Kiswahili.
Akizungumza katika mahafali ya kupewa vyeti na kuagwa wanafunzi waliojifunza katika Skuli hiyo katika kampasi ya SUZA iliyoko Vuga, Bi Shani aliwashukuru wazazi wa familia walizokuwa wakiishi na wageni kwa kukaa nao vyema.
‘’Ahsante sana kwa kutuamini, ninaamini kwamba msaada huu hauko kwa walimu tu bali pia wazazi tunawashukuru sana kwa kutusaidia kuishi na wageni wetu vizuri’’,
Naye Mwalimu kutoka Chuo Kikuu cha Wit worth Marekani Megan alisema ameridhishwa sana na uongozi wa (SUZA) kwa kuwawezesha kusoma lugha ya Kiswahili katika mazingira mazuri ya darasani na familia walizokuwa wakiishi nazo.
Akitoa shukurani hizo,Megan alisema programu za kufundishwa Kiswahili zimekuwa zikiratibiwa vyema kwa muda mrefu na kuahidi kuwa wataendelea kuwa pamoja katika kuendelea kuikuza lugha ya Kiswahili.
Aidha, alizitaja familia ambazo wanafunzi walikuwa wakiishi nazo pia zimetoa mchango mkubwa wa maendeleo yao sambamba na kuwafundisha mambo mengine ya utamaduni wa Mswahili.
Wakitoa shukurani zao katika maonesho madogo madogo ya kuzungumza kama kama michezo ya kuigiza mbele ya wageni katika mahafali hayo walieleza kufurahishwa kwao na jinsi walivyojifunza na kuishi katika familia.
‘’Tumefurahi kuwa na uzoefu mkubwa katika lugha, tunadhani kiswahili chetu kimekuwa kwa mfano hivi sasa tuna uwezo wa kusoma vitabu, tunapambana na tunatarajia tutaweza kufanikiwa zaidi’’, alisema mwanafunzi
Katika masomo hayo pia wanafunzi 15 waliohitimu masomo yao ya mwezi mmoja walipata fursa ya kutembelea maeneo yakiwemo ya kihistoria na yakiwemo ya Jozani, Jambiani, Kizimbani, Maruhubi na Kijichi, CHAKO na Nungwi,