MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Ali Suleiman ametoa wito kwa vijana kutumia fursa zinazowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili waweze kuzalisha mazao na kukuza ufugaji nchini.
Aliyasema hayo katika ufunguzi wa maonesho ya Kilimo yanayoendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba huko Chamanangwe aliyahimiza mabaraza ya vijana kutumiwa kwa tija ili yawe mkombozi wa nchi yao katika kukuza uchumi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 ikiongozwa na mipango mbali mbali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kuwekeza katika kilimo chenye tija cha mazao ya chakula na biashara ambacho kitawaongezea kipato.
Katika hatua nyengine, Mhe. Suleiman alisema kuwa kuna fursa nyingi za vijana kujiajiri hasa kufuatia meli kubwa ya mizigo kufunga nanga katika bandari kisiwani Pemba.
‘’Tuna fursa nyingi za kujiajiri, bandari ya iliyokuwa inapakua makontena kutoka 30 hadi 60 sasa kuna oda ya zaidi ya makontena 600 yanataka kuletwa huku oda nyengine zinamiminika’’, alisema.
Aidha, alizungumzia uimarishwaji wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ambayo ni fursa nyengine ya kuwawezesha wakulima kutumia barabara kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za kilimo na kuwawezesha kuyafikia maeneo wanayohitaji kwa ufanisi.
Aidha, aliongeza kuwa fursa zinazokuja za vijana Serikali itaendelea kuwasimamia na kuwahimiza kufanya kazi kwa pamoja kwa manifaa ya taifa lao.
Aliongeza kuwa serikali imejenga miundo mbinu ya umwagiliaji katika mabonde sita ya mpunga Jendele, Chaani, Kibokwa iliyohusisha mabwawa makubwa na madogo ambayo yataongeza kilimo chake kwa mwaka.
Aidha, katika maonesho hayo, Mhe. Suleiman alikabidhi vitabu vya matokeo ya utafiti wa kilimo kwa miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika maonesho hayo.
Mapema, Waziri wa Kilimo Umwagiliaji, Maliasiali na Mifugo, Mhe, Ali Abdallah Shamata alisema ujumbe wa mwaka huu ni; Haki Kupata Chakula kwa Maisha Bora ya Sasa na Baadae unalenga kuongeza maarifa kwa wakulima, kuimarisha lishe kipato, kupata tija na kipato kwa uchumi wa Taifa.
Alieleza kuwa Mpango wa mageuzi wa Sekta ya Kilimo na mipango mbali mbali mikakati ya nchi sambamba na Ilani ya CCM ya 2025 vyote vinalenga kuimarisha sekta hii.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndg. Ali Khamis alisema hii ni mara ya kufanyika maonesho katika viwanja vya Chamanagwe ambapo mwaka huu taasisi 130 kutoka Tanzania Bara na Visiwani zimeshiriki kuonesha teknolojia na utaalamu wao katika sekta ya kilimo.
Maonesho yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali, mke wa makamu wa Pili wa Rais, mama Sharifa Omar, taasisi za Serikali ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na taasisi za binafsi kutoka Tanzania bara na Zanzibar na wananchi wa mikoa yote miwili ya kisiwa cha Pemba.
Hivi karibuni, Makamo Mkuu wa SUZA, Prof: Moh’d Makame Haji alisema Chuo kimeanzisha utaratibu maalum wa kuwapatia elimu wanafunzi itakayowawezesha kujiajiri ikiwa ni azma ya kutekeleza mipango ya Serikali ya kupambana na umasikini.
Kupitia mikakati mbali mbali iliyojiwekea ya kuleta mabadiliko ya jamii kupitia elimu, Chuo kimekuwa kikiandaa shughuli mbalimbali za kunufaisha jamii na wananchi wake.
Kwa kutumia mbinu hizi, wana SUZA na wanajamii wanapata fursa ya kukaa pamoja na kubadilishana mawazo sambamba na kujifunza mambo mengine ya kijamii katika jamii wanayoisimamia utekelezaji wa shughuli za kielimu kwa vitendo.
Prof. Haji alieleza kuwa Chuo kinatoa elimu kwa makundi kupitia Skuli ya Kilimo kupitia programu za kuwafikia wakulima waliopo Unguja na Pemba kupitia mradi wa TANRICE kwa kuwapatia elimu na mbinu bora za kilimo cha mpunga na mazao mengine.
Alisema kwa utumiaji wa mbinu hii, wanajamii wamefaidika na uzalishaji mkubwa wa mazao mbali mbali ya kilimo na biashara lakini wamejenga ukaribu wa kuelezea changamoto za kilimo kwa wataaalamu wa SUZA ambao huwafanyia ziara za kitaalamu mara mwa mara.