The State University Of Zanzibar

SUZA yajivunia utaalamu Maonesho ya  Sita  Chamanangwe

Wananchi kadhaa waliotembelea banda la maonesho ya Chakula yanayoendelea huko Chamanangwe mkoa wa Kusini Pemba wamevutiwa na utaalamu uliobuniwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa zanzibar (SUZA).

Miongoni  mwa jambo lililowavutia wengi na kuwa watulivu kupokea maelezo kutoka kwa mtaalamu aliyebuni teknolojia hiyo  Khamis Said Moh’d, mwanafunzi aliyemaliza Shahada ya Usimamizi wa Teknolojia ya Habari.

Mhitimu huyo alieleza kuwa  mfumo wa  banda la kufugia kuku    hutoa maji kutoka kwenye kisima kuingiza kwenye vyombo vya maji vilivyowekwa kwenye banda hilo kila yanapomalizika aidha, unaweza kurikodi kiwango cha maji yanayonywewa na kuku hao.

Aidha, mfumo wa chakula nao pia umebuniwa kuingiza kwenye vyombo katika banda la kuku bila ya kuhitaji mtu wa kuhudumia.

Alifafanua kuwa  mfumo mwengine ni  wa uingizaji wa hali joto kwenye banda hilo kwa mujibu wa mahitaji ya kuku ama vifaranga  vilivyowekwa  humo na pia  kurikodiwa ripoti zote zinazotumika hadi vifaranga vinauzwa au kuliwa.

Alielezea kuwa mfumo huo unasetiwa kuanzia kuku wanaowekwa wamegharimu kiasi gani, watatumia maji na chakula kiasi na hadi wanapotaka kuuzwa au kuliwa watakuwa kila kifaranga kitakuwa kimegharimu kiasi gani na   faida gani itakuwa imepatikana.

Mambo mengine ni  minazi ya muda mfupi iitwayo Red and Green Dwarf Malaysia Coconuts ambayo inaweza kuzalisha nazi kwa muda wa miaka mitatu.

Katika banda la SUZA pia kuna taaluma ya upandaji wa bustani ya jikoni ambayo imejegewa chanja , taaluma ambayo inapatikana pia katika mabanda mengine, pia bidhaa zinazozalishwa na Skuli  ya  Kilimo iliyoko Kizimbani Unguja.

Maonesho  ya Chakula Duniani mwaka huu yamezinduliwa leo (10/10/2024) huko Chamanangwe Mkoa wa Kusini Pemba  na Makamo  wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mhe. Hemedi Ali Suleiman yanatarajiwa kufungwa tarehe 19 mwezi huu. Yamepewa ujumbe wa  Haki ya Kupata Chakula  kwa Maisha Bora ya Sasa na Baadaye.