








17 Septemba 2026 | Oradea, Romania
Ujumbe wa Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), unaoongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Said Ali Hamad Vuai, umeendelea na ziara ya kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Oradea, Romania, kwa kutembelea Faculty of Economics pamoja na Faculty of Medicine and Pharmacy.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za SUZA za kuimarisha ujifunzaji wa kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kujifunza mifumo bora ya uendeshaji wa elimu ya juu, kwa lengo la kuboresha ubora wa elimu, kukuza ujuzi wa wanafunzi na kuongeza mchango wa Chuo katika maendeleo ya Taifa.
Katika ziara hizo, Uongozi wa SUZA umejifunza namna Chuo Kikuu cha Oradea kinavyobuni na kuendesha programu za masomo zinazozingatia mabadiliko ya teknolojia, mahitaji ya wanafunzi na mahitaji ya soko la ajira, ili kuwaandaa wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta mbalimbali.
Uchumi na Biashara
Katika Faculty of Economics, Uongozi wa SUZA umeangalia namna elimu ya uchumi inavyounganishwa na mahitaji ya biashara, ajira, ujasiriamali na uzalishaji, pamoja na namna wanafunzi wanavyoandaliwa kuwa wataalamu wenye uwezo wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Tiba na Famasia
Kwa upande wa Faculty of Medicine and Pharmacy, Uongozi wa SUZA umejifunza kuhusu mifumo ya mafunzo ya tiba na famasia, maendeleo ya taaluma, pamoja na mbinu zinazotumika katika kuwaandaa wanafunzi kuwa wataalamu wenye maarifa, ujuzi na weledi unaohitajika katika utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Ziara hii inaendelea kuimarisha dhamira ya SUZA ya kujifunza kutoka katika uzoefu wa taasisi za elimu ya juu kimataifa, kuimarisha uwezo wa kitaasisi na kuboresha programu za kitaaluma ili ziende sambamba na mahitaji ya wakati na maendeleo ya teknolojia.
Hatua hiyo pia inaendana na azma ya SUZA ya kuhakikisha uwekezaji katika elimu ya juu unazalisha rasilimali watu yenye maarifa, weledi, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto za jamii, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika elimu, utafiti na maendeleo.