





16 Septemba 2026 | Oradea, Romania
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Said Ali Hamad Vuai, leo ametembelea Skuli ya Uhandisi na Skuli ya Sayansi za Jamii katika Chuo Kikuu cha Oradea, Romania, ikiwa ni sehemu ya ziara za kitaaluma na kujifunza mifumo ya uendeshaji wa taasisi za elimu ya juu.
Ziara hiyo imelenga kutoa fursa kwa uongozi wa SUZA kupata uzoefu wa moja kwa moja kuhusu mifumo ya kitaaluma, kiutawala na kiutendaji inayotumika katika Chuo Kikuu cha Oradea, hususan namna chuo kinavyounganisha programu za masomo na mahitaji ya sekta, ubunifu, uzalishaji na mabadiliko ya soko la ajira.
Katika ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo amepata fursa ya kujifunza namna Chuo Kikuu cha Oradea kinavyobuni na kuendesha programu za masomo zinazozingatia mahitaji ya wanafunzi, waajiri na sekta mbalimbali, huku kikilenga kuwajengea wahitimu maarifa, ujuzi na uwezo unaohitajika katika ushindani wa soko la ajira la ndani na kimataifa.
