The State University Of Zanzibar

TCU yashauri mafunzo ya vitendo

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania  (TCU),  Prof. Charles Kihampa amewahimiza wakuu wa Skuli za  Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuwafundisha wanafunzi wao  kwa vitendo ili wakiajiriwa watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

 Hayo aliyasema  wakati akizungumza na Wakuu wa Skuli na Wakurugenzi wa SUZA kwenye kikao kilichofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya SUZA yaliyopo Tunguu mkoa wa Kusini Unguja tarehe 09/01/2026, hivi sasa ulimwengu umebadilika hakuna taasisi hata moja inayoajiri mfanyakazi kisha ikaanza kumsomesha.

‘’Anayeajiri anakuwa na matumaini hivyo, mnapowafundisha wanafunzi hakikisheni wanafanya mazoezi ya kikweli kwani muajiri hana muda huo, anahitaji akimchukua awe anajua kila kitu,’’alisisitiza.

Alieleza kuwa wanafunzi wafundishwe kwa kupewa taaluma ya kutosha na kutoa mfano wa mwanahabari akiajiriwa awe anafanya kikamilifu.

Aidha, aliupongeza uongozi wa  Taasisi ya Utalii  Maruhubi  kwa kuwafundisha wanafunzi wao kutandika vitanda, kupika na kuwahudumia  wageni huku wakiwa wanasimamiwa na mwalimu wao

Prof. Kihampa alieleza kuhusiana na ziara yake kuwa alifika SUZA kufuatia mabadiliko ya uongozi wa  kwenye Chuo ili kutoa ushauri wa namna bora ya  Chuo kutekeleza  majukumu yake.

Alieleza kuwa  wajibu wake  kuishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kama anavyowajibika kwa Wizara kama hii Tanzania Bara  na hata taasisi za elimu za binafsi.

‘’ Sisi kazi yetu si kusubiri mambo yaende sivyo ndio tuingilie kati, hapana’’, alieleza.

Alifafanua kuwa ili mambo yaende vizuri ni vyema  kila jambo lifanyike kwa utaratibu uliowekwa  na mambo yaliyopitishwa ni lazima yatekelezwe.

Kikao hicho kilichoongozwa na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa SUZA anayeshughulikia masuala ya Fedha, Mipango na Utawala, Prof. Salum Seif Salum kilitoa fursa ya washiriki kufahamu hoja mbali mbali zilizopata majibu ya Prof. Kihampa.

Akitoa shukrani zake, Prof. Salum alisema wamefarijika sana na ziara hiyo hasa kwa kushauriwa mambo mbali mbali  na kuwa na matumaini makubwa kuhusu mitaala iliyowasilishwa TCU kwa ajili ya kuthibishwa itakamilika mapema ili iweze kuanza mwaka ujao wa masomo.
https://www.instagram.com/p/DTSaaAmiAJg/?igsh=MWY4cTZpd3ZpZ3cyaQ==