The State University Of Zanzibar

Serikali yaongeza bajeti mikopo elimu ya juu

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar(SUZA) Dkt. Hussein Mwinyi   amefahamisha kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Shilingi bilioni 33.3 mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Shilingi bilioni 37.94 mwaka 2025/2026.

hayo aliyasema hayo  tarehe  20 Disemba 2025 alipohutubia kwenye  Mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), yaliyofanyika  Ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema  hatua hiyo imechangia kuongeza idadi ya  wanafunzi waliopata mikopo upande wa Zanzibar   kutoka wanafunzi 1,093 mwaka 2024/2025 hadi wanafunzi 1,725 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 63.

Dkt Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema ubora wa elimu ya juu ni alama  ya maendeleo ya Taifa ambayo ina uwezo wa kuzalisha  wataalamu   wanaoweza kuhimili changamoto za Karne ya 21  za sayansi na teknolojia.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ameupongeza uongozi wa SUZA pamoja na wahadhiri kwa juhudi zao za kutoa elimu bora na kukifanya chuo hicho kuwa kichocheo cha mabadiliko ya jamii kikiwa ni na miongoni mwa vyuo vinavyotambulika katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa SUZA kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za jamii na kuinufaisha Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali.

Naye kaimu Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Abdi Taliba Abdalla alisema wahitimu 2,536 wametunukiwa shahada katika ngazi mbalimbali ikiwemo vyeti,  stashahada, shahada za uzamili na shahada za uzamivu kwa mwaka wa masomo 2024/2025 miongoni mwo wanawake ni 1,614 na wanaume ni 922.