











CHUO Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) kimetoa mafunzo maalum ya Itifaki ya viongozi wa kitaifa ili kuimarisha uandaaji na uendeshaji wa Mahafali ya 21 yanayotarajia kufanyika tarehe 20 mwezi.
Akitoa mafunzo hayo kwa Kamati ya Itifaki (Kamati ya ukaribishaji wageni) ya Mahafali ya 21 ya SUZA katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein uliopo Kampasi ya Tunguu, mkoa wa Kusini Unguja, Naibu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ndg. Alison Chaula alisema SUZA inapaswa kufuata miongozo ya ukaribishaji viongozi wa kitaifa ili kuendesha shughuli hiyo kwa ufanisi.
Alifahamisha kuwa ni vyema kwa taasisi yoyote itakayoandaa shughuli inayowashirikisha viongozi wa kitaifa kuzingatia utaratibu sahihi wa kuwaalika viongozi wa kitaifa, uandaaji wa kadi, uandishi sahihi wa mabango ya sherehe, utambuzi wa hadhi na vyeo vya viongozi wa kitaifa, sambamba na usahihi wa maeneo waliyoandaliwa kukaa viongozi wa kitaifa katika shughuli husika.
Akitoa shukurani baada ya mafunzo hayo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa SUZA anayeshughulikia masuala ya Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Salum Seif Salum alisema SUZA imeyazingatia maelekezo na miongozo iliyotolewa kwenye mafunzo hayo na imeahidi kushirikiana na Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki ili kuboresha Mahafali ya 21 katika kufuata Itifaki kwa viongozi wa kitaifa. Mafunzo hayo yanajiri kuafuatia maandalizi ya Mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar SUZA yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi Disemba 20 mwaka huu katika kumbi wa Dkt Ali Mohammed Shein kampasi ya Tunguu.