The State University Of Zanzibar

Kongamano la Kitaaluma na Uzinduzi wa Hifadhi ya Kidijitali ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane imefanikiwa kutekeleza falsafa  ya R4 inayolenga Mageuzi ya Kiuchumi, Kielimu, na Kijamii kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika Kongamano la Kitaaluma na Uzinduzi wa Hifadhi ya Kidijitali ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar katika ukumbi wa Dkt Ali Mohamed Shein Mkoa wa Kusini Unguja Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yanayochochea ubunifu, elimu bora, na ujenzi wa uchumi wa kidijitali unaowaunganisha wananchi wote huku akiwataka wananchi kuendeleza amani na mshikamano uliopandikizwa na waasisi wa taifa hili. Aidha amebainisha kuwa misingi ya uongozi wa muasisi wa zanzibar, hayati sheikh Abeid Amani Karume, ilijikita katika kuhimiza uzalendo, haki na umoja wa wananchi, misingi ambayo serikali ya sasa imeendelea kuitekeleza kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Kitaaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume Prof. Eginald Mihanjo amesema ipo haja ya serikali kuanzisha vyuo maalum vitakavyolenga kuandaa viongozi imara na wenye maadili mema. Amesema viongozi wengi wa sasa wanakosa mafunzo ya uongozi wa kizalendo na utumishi wa umma unaojali maslahi ya wananchi, jambo linalohitaji kurekebishwa kupitia elimu maalum ya uongozi.

Naye  Makamu Mkuu Wa Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d  Makame Haji, amesema kongamano hilo halikuwa tukio la kitaaluma, bali ni jukwaa muhimu la kutafakari historia, falsafa na urithi wa kipekee wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Kongamano hilo na Uzinduzi wa Hifadhi ya Kidijitali ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar lenye Kauli mbiu “Maisha ya Sheikh Abeid Amani Karume na Urithi kwa Vijana: Amani, Mshikamano, na Demokrasia Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kigoda cha Kitaaluma cha Sheikh Abeid Amani karume kilianzishwa mwaka 2024 na Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) chenye lengo la kufanya  tafiti, mihadhara na mijadala ya kitaaluma kuhusu maisha, falsafa na mchango wa muasisi huyo katika kurithisha vizazi vya sasa na vijavyo.