


Naibu Makamu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdallah, amewataka wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kutumia rasilimali za Chuo kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla badala ya kuzitumia kwa maslahi yao binafsi.
Prof. Abdi Talib Abdallah alitoa wito huo wakati wa kikao chake na Mkuu wa Skuli ya Biashara pamoja na Wakuu wa Idara wa Skuli hiyo kilichofanyika katika kampasi ya Chwaka, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake, Prof. Abdi Talib Abdallah alisisitiza kuwa serikali na jamii kwa ujumla ina matarajio makubwa kutoka kwa SUZA kama nguzo muhimu ya kitaaluma na maendeleo ya taifa, hivyo ni wajibu wa wanataaluma kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Chuo na taifa.
“Ni muhimu kila mmoja wetu kufanya kazi kwa niaba ya chuo na si kwa faida binafsi. Tujitahidi kutumia maarifa na rasilimali tulizonazo kwa njia ambayo italeta tija kwa SUZA na jamii inayotuzunguka,” alisisitiza Prof. Abdi Talib Abdallah.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa skuli hiyo kumpa ushirikiano katika kipindi chake cha uongozi kama Naibu Makamu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, ili kwa pamoja waweze kuinua viwango vya taaluma na maendeleo katika Chuo hicho.
Katika kikao hicho pia, Prof. Abdi Talib Abdallah alipokea changamoto mbalimbali zinazokabili Skuli ya Biashara na kuahidi kuzifanyia kazi. Alibainisha kuwa changamoto zilizoko ndani ya uwezo wake kama kiongozi atazitatua mara moja, huku zile zinazohitaji maamuzi ya juu zaidi atazifikisha kwa uongozi wa Chuo kwa ajili ya majadiliano na hatua stahiki.
Kwa ujumla, kikao hicho kililenga kuimarisha mawasiliano baina ya uongozi wa SUZA na watendaji katika skuli, pamoja na kujenga mazingira bora ya utendaji kazi kwa lengo la kukuza ubora wa elimu na huduma zinazotolewa na SUZA.