



Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeeleza dhamira yake ya dhati ya kuimarisha shughuli za utafiti kwa njia ya kitaasisi, na kuachana na mtindo wa tafiti za mtu mmoja mmoja zisizo na mwelekeo wa pamoja. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Makamu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdalla, wakati wa uzinduzi wa mafunzo maalum ya utafiti kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyofanyika katika Kampasi ya Taasisi ya Utalii, Maruhubi.
“Tunatakiwa kujitoa kikamilifu kwa sababu moyo wa chuo ni kufanya utafiti zenye tija. Toka nifike hapa SUZA, nimegundua tafiti nyingi zinafanywa binafsi badala ya kufanywa kama taasisi. Hili tunahitaji kulibadilisha,” alisisitiza Prof. Abdi Talib Abdalla.
Prof. Abdi Talib Abdalla alieleza kuwa chuo kinakusudia kurejesha jarida lake la kitaaluma (JONO) ambalo litakuwa la viwango vya juu, na kulifananisha na mtoto wa ng’ombe anayezaliwa na kuanza kutembea ndani ya muda mfupi, akimaanisha kuwa jarida hilo litakuwa na maendeleo ya haraka na kuwa na mchango mkubwa katika kupandisha vyeo vya wakufunzi na kutatua changamoto za kitaaluma.
Aidha, alitangaza mpango wa SUZA kufungua kampuni maalum itakayosaidia kuendesha baadhi ya miradi ya utafiti kwa njia ya kibiashara ili kusaidia chuo kujitegemea kiuchumi.
“Lazima tujiwekee viwango vya juu. Hatuwezi kuendelea kuchapisha tafiti zetu kwenye tovuti zisizo na ubora. Tunahitaji kuchapisha katika majarida yenye hadhi,” alisema Prof. Abdi Talib Abdalla.
Katika kuimarisha ushiriki wa jamii ya SUZA katika tafiti, aliwataka watafiti wote kuhakikisha wamejiunga na Google Scholar ili kuongeza mwonekano wa kazi zao na kuhamasisha ushirikiano kati yao na wataalamu wa teknolojia ya habari (IT) kwa matokeo bora zaidi.
Kadhalika, alisisitiza umuhimu wa kutumia wanafunzi vizuri katika tafiti zao, akitoa wito kuwa kila mwanafunzi anayefanya utafiti, lazima aweze kuchapisha angalau karatasi (paper) moja ya kisayansi.
“Leo hii tunapaswa kuifanya SUZA isionekane tu kama kituo cha elimu, bali pia iwe ni kituo cha utafiti kwa manufaa ya chuo chenyewe, serikali na jamii kwa ujumla,” alihitimisha Prof. Abdi Talib Abdalla kwa msisitizo.
Kwa niaba ya wanataaluma walioshiriki mafunzo hayo, Dkt. Abubakar Makame Fakih alimshukuru Naibu Makamu huyo kwa ufunguzi wa mafunzo hayo muhimu na kuahidi kuwa watazingatia yale yote waliyoelekezwa na kuyafanyia kazi kwa vitendo.