




Katika juhudi za kukuza maarifa ya tabia nchi miongoni mwa vijana, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa mashirikiano na African Institute for Mathematical Sciencies (AIMS), leo kimeandaa mafunzo maalum ya siku moja kwa wanafunzi wa sekondari, yaliyofanyika katika ukumbi wa SUZA, KAmpasi ya Vuga. Mafunzo hayo yaliyozikutanisha skuli nne kutoka Unguja.
Akifungua rasmi mafunzo hayo tarehe 2 Oktoba 2025, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Prof. Moh’d Makame Haji alitoa wito mzito kwa wanafunzi hao, akisisitiza kuwa serikali ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahitaji wataalamu lakini sio wataalamu wa ndani ambao ndio miongoni mwao.
“Serikali inawahitaji nyinyi,” alieleza kwa msisitizo, “na muda wa kujiandaa ni sasa.”
Akigusia historia ya elimu Zanzibar, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji alisema kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya elimu ya juu. Wakati huo, mwanafunzi aliyemaliza sekondari na kufaulu, ilibidi kusafiri nje ya nchi kutafuta elimu ya chuo kikuu jambo ambalo mara nyingine lilikwamishwa na hali duni ya kifedha. Hata hivyo, hali imebadilika. Leo, Zanzibar inajivunia kuwa na vyuo vikuu vyenye hadhi, na SUZA ikiwa kinara katika kutoa elimu ya juu ya kisasa.
“Leo hii, mwanafunzi ana nafasi ya kuchagua chuo na kozi anayopenda hapa hapa nyumbani,” alisema, Prof. Moh’d Makame Haji.
Pia alitaja mfano wa baadhi ya wanafunzi wa SUZA waliopata fursa ya kwenda Marekani hivi karibuni kwa ajili ya kujifunza taasisi ya NASA , akieleza kuwa hilo ni ushahidi wa wazi kuwa mafanikio yanawezekana kwa mwanafunzi anayejituma. Aliwahimiza wanafunzi wa sekondari kutumia ipasavyo fursa zilizopo sasa ili waweze kufikia mafanikio ambayo huko nyuma hayakuwa rahisi kupatikana.
Prof. Moh’d Makame Haji. Amesema kwa sasa SUZA imeandaa mitaala yenye mwelekeo wa kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri baada ya kuhitimu, badala ya kutegemea ajira pekee.
“SUZA haifundishi kwa ajili ya vyeti tu,” alisisitiza. “Tunawajenga vijana kuwa wabunifu, wenye uwezo wa kuanzisha miradi na kujiajiri.”
Makamu Mkuu huyo pia alikiri kuwa serikali zote mbili ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar zinaendelea kuwaunga mkono wanafunzi wa elimu ya juu kwa kuwapatia mikopo, lengo likiwa ni kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyoweza kukwamisha safari yao ya kielimu.
Kwa upande wake, Dkt. Ghafi Konde Akara, mwakilishi kutoka shirika la kimataifa la mazingira Ikirere alipongeza SUZA kwa hatua kubwa waliopiga katika kutoa elimu bora. Aliwapongeza pia kwa mazingira bora na rafiki ya kujifunzia, akisema ni mfano wa kuigwa.
Aliwatia moyo wanafunzi waliopata nafasi ya kushiriki katika mafunzo hayo ya siku moja, akiwahimiza kutumia kipindi hiki kuchagua mwelekeo sahihi wa maisha yao ya baadaye.
“Mna bahati kubwa kuwa katika wakati sahihi,” alisema. “Chagueni kitu mnachokipenda, na anzeni kukijengea msingi mapema.”
Mafunzo haya ya siku moja yamehusisha wanafunzi kutoka skuli nne ambazo ni: Hasnuu Makame, Ben-Bella, Lumumba, Dkt. Ali Mohammed Shein.