The State University Of Zanzibar

SUZA Yawakirimu Walimu 16 Kutoka Igunga katika Ziara ya Kitaaluma

Jumla ya walimu kumi na sita (16) kutoka Shule ya Sekondari Igunga, iliyopo Mkoa wa Tabora, Tanzania Bara, wametembelea Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar – SUZA, ikiwa ni sehemu ya juhudi za chuo hicho kujitangaza na kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka Tanzania Bara na nje ya nchi.

Ziara hii ni matokeo ya kampeni za maafisa wa udahili wa SUZA wanaozunguka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu juu ya fursa zinazopatikana chuoni hapo. Walimu hao walipokelewa kwa ukarimu na Naibu Makamu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Uendeshaji, Dkt. Hashim Hamza Chande.
Katika Salamu yake ya kuwakaribisha, Dkt. Chande alisema:

“Karibuni sana Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar – SUZA. Jihisini mpo nyumbani.”
Aliongeza kuwa SUZA inaendelea kukuza ushirikiano na shule mbalimbali ili kuhamasisha wanafunzi kujiunga na suza”
Aidha, aliwafahamisha walimu hao kuwa SUZA ina jumla ya skuli tisa, ambazo ni:
• Skuli ya Biashara
• Skuli ya Utalii
• Skuli ya Afya
• Skuli ya Kilimo
• Skuli ya Kompyuta na Habari
• Skuli ya Meno
• Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni
• Skuli ya Elimu
• Skuli ya Benjamin Mkapa (iliyopo Pemba)

Mbali na kutembelea chuo, walimu hao pia walipata fursa ya kuzuru maeneo ya kihistoria ya Zanzibar, ikiwemo Makumbusho ya Bunge kwa Bihole, pamoja na Msikiti wa Kihistoria wa Kizimkazi.
Ziara hii imeonesha mafanikio ya juhudi za SUZA katika kufungua milango kwa wanafunzi kutoka pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nje ya nchi, huku walimu wakielezea kufurahishwa kwao na mapokezi pamoja na ubora wa mazingira ya kujifunzia chuoni hapo.