The State University Of Zanzibar

Prof. Haji Wataalamu Wajiamini ili Kujenga Taifa Imara

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Makame Haji, ametoa wito kwa wataalamu wa ndani kujenga imani binafsi na kutumia maarifa yao kwa tija, akisisitiza kuwa ujasiri wa kitaaluma ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.

Akizungumza katika warsha ya Maendeleo ya Maabara ya Usanifu wa Vinasaba iliyofanyika katika Skuli ya Sayansi ya Afya na Sayansi za Tiba, kampasi ya Mbweni, Prof. Haji alieleza kuwa SUZA imekuwa kinara katika kuandaa wataalamu kupitia mradi wa kimataifa wa Strengthening Capacity to Manage and Cope with Pandemics in Ethiopia and Tanzania (SCCOPET).

“SUZA imewafundisha wataalamu ndani na nje ya nchi, wakiwemo wasiokuwa wa SUZA, kwa makubaliano ya kushirikiana katika tafiti, usimamizi wa wanafunzi, na utoaji wa mafunzo. Hii ni njia ya kujenga mtandao wa kitaaluma unaoleta tija kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Haji.

Hata hivyo, Prof. Haji alielezea masikitiko yake juu ya baadhi ya watumishi wa umma wanaopuuza fani zao na kushindwa kutumia mafunzo yao kwa manufaa ya jamii.
“Serikali inatumia gharama kubwa kuwaandaa vijana katika fani adimu ili walete mabadiliko. Lakini baadhi yao wanashindwa kuleta maendeleo yaliyotarajiwa,” aliongeza.

Warsha hiyo iliwakutanisha wataalamu wa maabara kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo: Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Idara ya Utafiti ya Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Kitengo cha Malaria, Wakala la Maabara na Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Sumeit, Skuli ya Kilimo ya Zanzibar, Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji na Maliasili, Taasisi ya Maradhi Yasiyoambukiza, Wakala wa Chakula na Dawa na Maabara ya Afya ya Jamii.

Warsha hii ni sehemu ya juhudi za SUZA kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kushirikiana na wadau wa sekta ya afya katika kukabiliana na changamoto za maradhi ya mripuko na kuendeleza tafiti bunifu kwa maendeleo ya jamii.