The State University Of Zanzibar

Ushirikiano SUZA, ACU kufungua fursa za kitaaluma

Naibu Makamu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Fedha, Mipango na Utawala wa Chuo Kikuu cha taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Hashim Hamza Chande, ameushukuru Umoja wa Vyuo Vikuu vya Jumuia ya Madola (The Association of Common Wealth Universities – ACU) kwa mchango mkubwa wa kitaaluma inayoendelea kuitoa kwa SUZA.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumkaribisha Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Kijamii, Dkt. Laura Pritsch kutoka ACU, katika ofisi za makao makuu ya SUZA Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 9/07/2025, Dkt. Chande alisema SUZA imefaidika kwa kuwa na wanafunzi kadhaa wanaofaidika na ufadhili masomo wa Umoja huo.

‘’Tunawashukuru sana, ACu wana fursa nyingi tunazohitaji kwa wanafunzi na watendaji kujengewa uwezo’’, alisema.

Naye Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Kijamii, Dkt. Laura Pritsch kutoka Umoja wa Gyuo Vikuu wa Jumua ya Madola alisema ACU ina fursa nyingi miongoni mwao zinatolewa kwa njia online kwani si kila mmoja anaweza kusafiri kutafuta elimu.

“Ninapendelea sana wanafunzi wa SUZA watumie fursa hii, tungependa pia kupata mwakilishi wa SUZA ili kuzipeleka ajenda zao kwenye kikao kikao kikuu, kitakachofanyika mwakani’, alisisitiza Dkt. Pritsch.

Aliongeza kuwa Umoja huo unazishawishi nchi wanachama kuchangia ili wanafunzi wengi waweze kujiunga na masomo hayo.

Mapema, Kaimu Mkurugenzi wa Shahada za Juu, Utafiti na Ushauri Elekezi Dkt. Miza Ali Kombo, alisema Umoja huo umewawezesha wanafunzi watano kufaidika na mpango wa masomo ambapo wanafunzi wengine wawili wanaendelea na masomo yao.

Vilevile, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar, Dkt. Abdalla Ibrahim aliwahimiza wanafunzi kuomba fursa za masomo zinazotolewa na Umoja huo kwani ni fursa ghali sana kupatikana katika maeneo mengine.

Alizitaja miongoni mwa fursa hizo kuwa ni pamoja na program za masuala ya mazingira, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Naye Ofisa uendeshaji Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu Taaluma, Ndg. Abdallah Ahmed Suleiman aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Umoja huo kwa SUZA aliahidi uteuzi wake utachangia kuchangamkia fursa za kitaaluma kwa wanafunzi wa SUZA.

‘’Tutaunganisha mawasiliano na utekelezaji wa maazimio yanayopitishwa na SUZA kuhusu fursa za masomo ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kukutana na wanafunzi wa nchi nyengine waliofaidika na Umoja huu’’, alisema.

Aidha, mwanafunzi mnufaika wa ufadhili wa Umoja huo ambaye anaendelea na masomo yake ya Shahada ya Uzamili ya Elimu kwa Vijana, Jinsia na Maendeleo, Ndg. Mansour Jalou kutoka Sierra Leone alisema amekichagua Chuo hiki ili aendelee na masomo yake kwa sababu mfumo wao wa utoaji wa elimu umemvutia.

‘’Mfumo wa elimu umenivutia, ni SUZA pekee ambao wanatoa programu hii katika Vyuo vilivyoko kwenye Umoja huu’’, alisema.

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar ni mwanachama wa Umoja huu tangu mwaka 2019 na kinaendelea kunufaika na fursa nyingi za Umoja huo wenye wanachama zaidi ya 400 wengi wao ni kutoka nchi za Afrika.