The State University Of Zanzibar

Kiswahili kimeunganisha Watanzania-BAKIZA

MWENYEKITI wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, Bi Saade Said Mbarouk, amesema watanzania wana tunu adhimu ya kujivunia inayoendelea kuwaunganisha katika harakati zao zote za maisha, licha ya kuwepo makabila mengi na lugha zao.


Akizungumza katika shamrashamra za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani zilizofanyika kwenye kwenye kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) huko Nkurumah, Mkoa wa Magharib ‘A’ tarehe 4/07/2025, alisema hazina ya Lugha hii ya Kiswahili ilipatikana mara tu baada ya Uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita ambapo imeendelea kukua na kuipatia umashuhuri Tanzania pamoja na watu wake.
‘’ Baada ya Uhuru wa Tanganyika, jambo la kwanza ambalo hayati Mwalimu Nyerere alilifanyia kazi ni kuwaunganisha watanzania kwa kukitangaza Kiswahili kuwa lugha ya Taifa, licha ya kuwepo makabila na lugha zao zaidi ya 200 ’’, alisema Bi Saade.

Aidha, aliongeza kuwa hayati Mwalimu alihakikisha kuwa lugha hiyo inatumika katika harakati za kisiasa za kuleta Uhuru kwa nchi jirani za Tanzania.


Hivyo, alisisitiza siku hii ikumbukwe sambamba na viongozi ambao walitoa mchango mkubwa kukikuza Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Afrika ambako vituo maalum vya kuiendelea lugha hii vimefunguliwa.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti huyo alitoa wito wa matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kwa wanahabari, wanataaluma na wadau wengine badala ya kukibomoa na kukichafua.


Mapema, Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Kiswahili na Lugha za Kigeni na Kituo cha Taaluma na Uenezi iliyoko chini ya SUZA, Bi Zainab Ali Idd, alisema lugha ya Kiwahili inaendelea kukua kwa kasi duniani.


Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la KImataifa la UNESCO mwaka 2022, ilielza kuwa lugha ya Kiswahili inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani kote.


Alizitaja nchi kama vile, Libya, Zambia, Morroco, Algeria na nyengine zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa ni miongoni mwa nchi zilizopania kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zao nyingi.
Naye, Mkuu wa Idara ya Kiswahili, Dkt. Kijakazi Omar, aliwatanabahiha wadau wa lugha hii kuwa kuikumbuka siku hii, ili kuthamini fursa na kuendela na kukikuza Kiswahili katika nyanja za elimu, teknolojia, Sanaa.


Aidha, Ubalozi wa Tanzania nchini Japan ulianzishwa ‘Wiki ya Kiswahili Japan’ iliyoshiria namna lugha hii ilivyokua na inavyothaminiwa na mataifa mengine ambapo viongozi kadhaa na watendaji kutoka SUZA walialikwa.


Maadhimisho ya Siku hii ambayo yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 7/07/2025 yatafanyika Zanzibar kwa ushirikiano baina ya BAKIZA na Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA) la Tanzania.


Maadhimisho haya yamebeba kauli mbiu ya ‘Kiswahili kwa Amani na Mshikamano’ inayoashiria umuhimu wa kukuza amani na mshikamano katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 hapa Tanzania.
Katika kongamano hili, maonesho kadhaa ya kisanii yaliwasilishwa jukwaani ikiwa ni pamoja na nyimbo, utenzi, igizo, ushairi pamoja na nasheed iliyoelezea umuhimu wa lugha ya Kiswahili.