




CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kupitia Skuli Elimu Endelezi na Utaalamu (SCOPE), kimewatunuku vyeti wanafunzi 30 waliofaulu masomo ya IT, kompyuta na lugha katika masomo ya muda mfupi na mrefu.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika katika kampasi ya Vuga Mkoa wa Mjini Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mafunzo ya Habari, Skuli ya Kompyuta, Mawasiliano na Mafunzo ya Habari, Dk. Khamis Juma Abdalla, alisema mafunzo waliyoyapata ni muhimu kwa maendeleo yao na nchi kwa jumla.
“Tunahitaji kuwa na wataalamu wanaokwenda na wakati kwa kujifunza fani zitakazoleta ufanisi na kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar’’, alisema.
Aliongeza kuwa watu wengi wamekuwa wakitafuta wataalamu katika fani hii, jambo linaloonesha baada ya kumaliza masomo watafanikiwa kupata ajira.
Alisisitza kuwa fani za Lugha, IT na Kompyuta zimeshika kasi kwa kutumiwa na wataalamu katika sehemu nyingi za kazi hivyo ni vyema na wakazitumia ipasavyo.
Alifahamisha kuwa masuala ya lugha, IT na kompyuta ni fani ambazo zinahitaji mazoezi ya kuzifanyia kazi kwa vitendo ili kuleta ufanisi.
‘’Msikae mkajua nini maana ya lugha tu au IT utambuzi huo hautoshi kuwa umejifunza ila utumie taaluma hiyo kwa faida kwa faida yako na watu wanaokuzunguka’’,
Naye Ramia Mohammed Ramia kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, aliwakumbusha wanafunzi hao kutoridhika na elimu waliyoipata kwani haina kikomo.
“Ni lazima kila siku mtu ajitafutie namna ya kujiongezea elimu kwani kasi ya ukuaji wa elimu hasa katika teknolojia ni kubwa”, alisisitiza.
Alikumbusha wakati wa mripuko wa maradhi ya COVID 19 kuwa taasisi chache tu ndizo zilizokuwa zikifanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Aidha, Dk. Omar Ali Kombo ambaye aliwasilisha mada kuhusu ubunifu wa teknolojia katika kupeleka mbele maendeleo ya Zanzibar, alisema teknolojia inasaidia kusukuma mbele maendeleo katika nyanja nyingi licha ya nchi za Kusini mwa Afrika na Kati kutumia fani hiyo kwa kiwango kidogo.
Mapema mratibu wa SCOPE, Fatma Fakih aliwashajiisha wanafunzi kujiunga ma mafunzo hayo kwani yanatolewa mahususi kwa kumjenga mwanafunzi kutambua kutumia taaluma hiyo.
‘’Hata kama una shahada ya kwanza, njoo usome kwani tunatoa ujuzi ambao utakuwezesha kufanya kazi badala ya kupasi mitihani tu’, aliwakumbusha wahitimu hao.