The State University Of Zanzibar

SUZA NA CHUO KIKUU CHA OSAKA WAFUNGUA MILANGO YA MASHIRIKIANO

Katika ukingo wa dhahabu wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MAKISADU), leo tarehe 7 Julai 2025, historia imeandikwa upya. Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Osaka vimeweka saini Hati ya Ushirikiano, tukio hili likiashiria mwanzo mpya wa mashirikiano ya kitaaluma. Ghafla hii ya kusisimua iliyojaa uzuri wa lugha, sanaa, na utamaduni ilifanyika Osaka, Japani, na kuwavutia viongozi wa watu mbalimbali waliokusudia kufanikisha maono ya Kiswahili kama lugha ya ulimwengu.


Mkataba huu muhimu uliwekwa saini na Profesa Moh’d Makame Haji, Makamu Mkuu wa SUZA, na Profesa Yoshiki Yamamoto, Mkuu wa ISkuli ya Shahada za Ubinaadamu ya Chuo Kikuu cha Osaka. Katika hotuba yake ya shukrani, Profesa Moh’d Makame Haji alieleza kuwa “hatuna budi kukiri kuwa Vyuo vikuu ni kama taa zinazomulika njia za maelewano ya kimataifa — ni chemchem ya fikra, daraja baina ya mataifa, na ni mashamba ya maarifa yanayochipua ujuzi na hekima kwa vizazi vijavyo.

Ushirikiano wetu na Chuo Kikuu cha Osaka ni kielelezo cha diplomasia ya elimu, inayovuka mipaka ya jiografia na lugha, na kuleta muingiliano wa maarifa, utamaduni, na maendeleo endelevu. Ushirikiano huu wa kielimu utazalisha wataalamu, maarifa, na ubunifu wa kisayansi, huku ukikuza maingiliano ya nchi kupitia utalii wa makongamano na shughuli za kisayansi, kitamaduni, na uwekezaji.”


Kwa maneno haya yaliyojaa hekima, Profesa Moh’d Makame aliendelea kuonyesha umuhimu wa tarehe hii adhimu, akisema: “Ni fakhari kubwa kwetu sote kuona tukio hili la kihistoria limefanyika leo, tarehe 7 Julai, siku ambayo Kiswahili ni moja ya lugha chache barani Afrika zilizopewa hadhi ya urithi hai wa lugha na Shirika la UNESCO. Lugha hii adhimu, inayopumulia upepo wa Bahari ya Hindi, si tu chombo cha mawasiliano, bali ni tanuri la utambulisho wetu kama Watanzania, Waafrika, na kama walimwengu.”
Kwa msisitizo wa dhati, alihitimisha kwa kusema: “Sisi tukiwa kitovu cha historia, fasihi, na uenezaji wa Kiswahili tunawajibika kuendeleza lugha hii kama silaha ya amani, daraja la utamaduni, na nyota inayoangaza Bahari ya Hindi hadi Pasifiki.”


Mkataba huu wa ushirikiano umejikita pia katika malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa lengo nambari 4, 8, 11, na 17, ambayo yanahimiza elimu bora, ajira na uchumi kupitia elimu, utalii wa makongamano, na ushirikiano wa kimataifa. Kwa pamoja, SUZA na Osaka wameweka msingi wa taaluma yenye kuleta maendeleo endelevu na kuhifadhi urithi wa kiutamaduni.


Katika ghafla hiyo, Balozi Baraka H. Luvunda alitoa matumaini yake kuwa ushirikiano huu utaimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa na kuchangia kueneza Kiswahili kama sarafu ya utamaduni. Vikundi vya sanaa vilipamba tukio hilo kwa utumbuizo wa kuvutia uliodhihirisha umahiri wa Waswahili katika nyimbo, ngoma, na ushairi.


Kwa maneno ya Kiswahili cha mwambao, “Ng’ombe wa maskini hazai, bali akipewa majani bora huzaa mapacha.” Vyuo hivi viwili sasa vimeweka msingi wa ufanisi wa vizazi vijavyo kupitia maarifa na maendeleo yanayozidi kuvuka pwani za Bahari ya Hindi.