The State University Of Zanzibar

SUZA, DMI wasaini hati kuimarisha mafunzo ya ubaharia

VIONGOZI wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Bahari cha Dar es Salaam wamesaini hati ya makubaliano kuongeza ushirikiano wa kitaaluma ya kutoa mafunzo ya ubaharia.


Utiaji saini huo ulifanyika kwenye ofisi za Makao Makuu ya SUZA yaliyoko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 26/06/2025 ambao uliwashirikisha wadau, watendaji na wataalamu katika sekta bahari.


Akizungumza katika hafla hiyo, Pro. Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji alisema dhamira ya kuanzisha taasisi hii ni ya muda mrefu ambayo ilitokana na asili ya watu Zanzibar ya kutumia rasilimali ya bahari katika uzalishaji bila kutumia utaalamu.

Aliongeza kuwa mazingira hayo yamechangia kuwaunganisha wazanzibari katika kazi za ubaharia.
‘’ Mazingira yamechangia kuwaunganisha watu kama vile aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, alifanya kazi hii kabla ya kujiunga na siasa’’, alifahamisha.


Aliongeza kuwa kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya matumizi ya raslimali hii hasa ikingatiwa kuwa waliowekeza kwenye seta hiyo wanapata faida kubwa kama vile Malaysia.


Katika kuelekea kwenye mafanikio hayo, SUZA imepeleka vijana kadhaa nje ya nchi kwa ajili ya kupata mafunzo ya muda mrefu na mfupi ikiwa ni pamoja na kupata taaluma ya uhandisi wa vyombo vya majini.


‘’Tunataka kuona program zetu zinajitosheleza kwa watakaofanya kazi za ubaharia’’, alisisitiza Prof. Haji.
Mkuu wa Chuo cha bahari cha Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo alisema taasisi yake imefarajika kuwa na washirika wanaotoa taaluma ya masuala ya bahari kwani imefanya kazi hiyo kwa muda mrefu ikiwa peke yake.


‘’ Tulikuwa peke yetu na kwa nguvu zetu hatukuweza kubeba mzigo wa Tanzania wa kutoa taaluma hiyo kwa sababu kuna uhitaji mkubwa na fursa zipo nyingi za kutumia rasilimali hiyo.’’ Alieleza Prof. Gurumo.
Alifahamisha kuwa Chuo hicho kilianza mafunzo ya ubaharia pekee kuanzia mwaka 1978 hadi ilipofika mwaka 2007 ndipo walipoanza kutoa mafunzo ya program nyengine.


Aidha, alifahamisha kuwa ana matumaini kuwa ushirikiano utachangia kupata watu wenye uweledi na ujuzi mkubwa kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa.


Katika kikao hicho, alieleza jinsi walivyofanikiwa kwa kushirikiana na vyuo vyengine duniani ambapo wamekuwa wakiendesha kongamano maalum la Uchumi wa Buluu kwa ushirikiano ambapo kwa mwaka ujao limepangwa kufanyika Zanzibar.


Mapema, Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Mafunzo ya Bahari ya SUZA, Bw. Yahya Hamad Sheikh alisema lengo la ushirikiano huo ni kuleta ufanisi zaidi kwenye maeneo ya kitaaluma na kiusalama.


Alisema hatua mbali mbali za kuimarisha utoaji wa taaluma zinaendelea kuchukuliwa kupitia mitaala ya mafunzo ya bahari yaliyowashirikisha wataalamu kutoka seta mbali mbali na kuwapatia mafunzo ya uhandisi vijana huko ughaibuni.