


Osaka, Japani — 1 Julai 2025
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimejitokeza kwa fahari kubwa kushiriki rasmi katika uzinduzi wa Juma la Kiswahili na Utamaduni uliofanyika jijini Osaka, Japani, ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Kibiashara la Kimataifa la Osaka 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Makamu Mkuu wa SUZA, Profesa Mohamed Makame Haji, alieleza kuwa wiki ya Kiswahili na Utamaduni itaendelea hadi tarehe 7 Julai 2025, ambayo pia ni siku ya maadhimisho rasmi ya lugha ya Kiswahili. Alisisitiza dhamira ya SUZA katika kuendeleza lugha ya Kiswahili na kutangaza utamaduni wake kimataifa.
“Kwa miaka mingi SUZA imekuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti, kufundisha, na kusambaza lugha ya Kiswahili pamoja na utamaduni wa Mswahili, na leo tunathibitisha dhamira yetu kwa kushiriki katika tukio hili la kihistoria kimataifa,” alisema Prof. Haji.
Katika kipindi cha wiki hii ya maadhimisho, matukio mbalimbali yamepangwa kufanyika yakiwemo maonesho ya utamaduni wa Mswahili.
Kilele cha juma hili kitashuhudia tukio la kihistoria la kutiwa saini kwa Mkataba wa Mashirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na Chuo Kikuu cha Osaka, hatua inayotarajiwa kufungua milango ya ushirikiano wa kisayansi, kitamaduni, na kitaaluma kati ya Tanzania na Japani.
Aidha, kutafanyika uzinduzi rasmi wa Kamusi Ndogo ya Kiswahili na Kijapani, kazi ya ubunifu iliyofanywa na wataalamu wa SUZA—Bi Shani Suleiman Khalfan na Fatma Soud Nassor—ikiwa ni mchango wa kuimarisha mawasiliano na uelewa wa kiutamaduni kati ya watu wa mataifa haya mawili.
SUZA inatoa wito kwa wadau wa elimu, lugha na utamaduni kuunga mkono juhudi hizi za kimataifa za kuikuza Kiswahili kama lugha ya maarifa, biashara na diplomasia duniani.