Makamo Mkuu wa Chuo Cha taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Makame Haji amesema Chuo kimeanzisha program mpya ya Shahada ya Tabibu Kinywa na Meno (Bachelor of Science in Doctor of Dental Surgery) ambapo kwa mara ya kwanza wahitimu watano wametunuliwa Shahada zao.
Akitoa salamu zake katika Mahafali ya 20 yaliyofanyika katika makao makuu ya SUZA Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja yaliyofanyika hivi karibuni, Prof. Haji alisema kati ya wahitimu hao watano wanawake ni wawili ambao ni sawa na wastani wa asilimia 40 na wanaume watatu sawa na asilimia 60.
‘’ Wahitimu hawa si tu wanawakilisha matunda ya kazi yetu ya pamoja, bali pia ni alama ya matumaini kwa maendeleo ya Zanzibar na nchi yetu kwa ujumla’’, alifafanua Prof. Haji.
Akizungumzia kuhusu ongezeko la wanafunzi kwa ujumla alieleza katika mwaka huu, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la wahitimu wanawake wanaofikia asilimia 61 ikilinganishwa na wahitimu wanawake waliofikia asilimia 58.46 mwaka 2023.
Akitoa ufafanuzi zaidi alisema kati ya wahitimu 2,291 mwaka huu, wahitimu 6 (3 wanaume na 3 wanawake) walitunukiwa Shahada ya Uzamivu, wahitimu 73 (26 wanaume, 47 wanawake) walitunukiwa Shahada za Uzamili, wahitimu 791 (323 mme, 468 w’ke) walitunukiwa Shahada za Kwanza, wahitimu 1095 (389 wanaume, 706 wanawake) walitunukiwa Stashahada, na wahitimu 322 (143 wanaume, 179 wanawake) walitunukiwa Astashahada (cheti).
Kutokana na mafanikio hayo SUZA itakuwa imezalisha wahitimu zaidi ya 19,000 tangu ilipoanza kazi ya kutoa taaluma miaka 24 iliyopita.
Aidha, alitumia fursa hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wa SUZA kuwapongeza wahitimumu wote kwa jitihada zao hadi kumaliza masomo yao kwa salama.
‘’ Ningependa kusema kwamba leo si mwisho wa safari ya elimu, bali ni mwanzo wa safari mpya. Wahitimu mnaendelea kuwa na jukumu la kuleta mabadiliko kwenye jamii yetu, taifa letu, na ulimwengu kwa ujumla’’, alisisitiza Prof. Haji.