Wengi wanaifunga safari ya kutafuta elimu wakipitia changamoto mbali mbali kukamilisha ndoto zao, lakini si wote wanaobahatika kufikia daraja ya kuwawezesha kupewa heshima kubwa katika tasnia hiyo.
Kauli hii inatufungulia ukurasa mpya wa wasifu wa maisha ya Mwalimu Haroun Ali Suleiman (71) katika sekta ya elimu uliomfungulia milango ya uongozi na uwajibikajika katika kazi hadi kufikia kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar mwaka 2025.
Si watu wengi waliokuwa wakimfahamu kuwa alifanya mambo mengi na makubwa kama yaliyosimuliwa zaidi ya dakika 40 wakati akiwa amesimama mbele ya hadhara ya wageni wa Mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Mwinyi.
Mwalimu Haroun alianza kazi mwaka 1976 akiwa mwajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na akiwa Mwakilishi katika jimbo la Makunduzi kuanzia mwaka 2000 hadi sasa.
Dk. Haroun anatajwa kuwa ni miongoni mwa magwiji wenye uzoefu kwenye utumishi wa umma, heshima ya kujituma na pia kuweka historia kubwa ya kupewa heshima ya kishika nyadhifa mbali mbali za uongozi kwa miaka 25 mfululizo katika awamu tano tafauti.
Pamoja kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia mwaka 1976 akiwa mwalimu wa skuli hadi mwaka 1992 bila kusita. Skuli alizowahi kufundisha ni Skuli ya Makunduchi (1976), Skuli ya Sekondari ya Benbella (1978), na Skuli ya Haile Sellasie (1979) ambapo wmaka 1985 alishika wadhifa wa Mwalimu Mkuu hadi mwaka 1992.
Mnamo mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uendeshaji wa Wizara ya Elimu na mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Mipango na Uendeshaji katika Wizara hiyo hiyo.
Kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na baadaye Wizara hiyo ilibadilishwa jina kufuatia kupewa jukumu la kutoa mafunzo ya amali kwa kuwapa vijana stadi za maisha ili waweze kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, hivyo iliitwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Mwaka 2010 hadi 2013 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kazi na Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na baadaye kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma hadi mwaka 2016.
Miaka miwili baadaye alipewa wadhifa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi na Utawala Bora ambapo kufuatia mabadiliko ya muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliteuliwa kushika cheo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi Umma na Utawala Bora.
Mmhadi kufikia kuteuliwa Waziri katika vipindi tafauti hadi sasa, Mwalimu Haroun ni chemchem ya kuanzishwa SUZA miaka 24 iliyopita.
‘’Uongozi umeona kuna haja ya kumtunuku Shahada ya uzamivu ya Heshima Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Katiba Sheria na Utawala Bora, Mwalimu haroun Ali Suleiman kutokana na mchango wake katika uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar ambao lengo kuu ni kuinua elimu ya Zanzibar.
Ushawishi huu uliibuliwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Salmin Amour Juma sambamba na wajumbe wengine kadhaa wakijumuika na mawaziri vinara wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika vipindi tafauti waliosimamia kuikuza fikra hiyo ni pamoja naye Mhe. Omar Ramadhan Mapuri, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee wakati huo akiwa Katibu Mkuu katika Wizara hiyo kwa kipindi kirefu alisimamia Kamati za Uratibu wa Uanzishwaji wa SUZA.
Akisoma wasifu wa Mwalimu Haroun, Naibu Makamu Mkuu SUZA masuala ya Fedha Mipango na Utawala, kwenye Mahafali ya 20 ya SUZA, Dk. Hashim Hamza Chande alisema alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa mwanzo waliaonzisha harakati Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, alijitolea kuhakikisha kuwa za zanzibar inapata Taasisi ya elimu ya Juu a itakayochangia katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
‘’Aliongoza juhudi za kutafuta wafadhili kutoka taasisi na Jumuia mbali mbali kimataifa kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) kupata fedha za ujenzi na miundombinu ya Chuo na kumshawishi aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Amani Abeid Karume kutumiwa eneo la Tunguuu (ambapo ndipo makao makuu ya SUZA),’’ alinukuu Dkt. Hashim.
Kutokana na jitihada hizo, Dk. Haroun alichangia kwa kiwango kikubwa kuwasaidia vijana wengi ambao walikuwa na hamu ya kujiunga na elimu ya juu kutimiza ndoto zao wakiwa nyumbani badala ya kutafuta vyuo nje ya nchi ambako walilazimika kutumia gharama kubwa kufanikisha azma zao.
Hadi kufikia mwaka wa masomo 2024/2025, SUZA itakuwa ikitoa program za mafunzo ya 57 katika ngazi ya Astashahada, Shahadaya Kwanza. Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu katika fani ya lugha, Sayansi, Utalii, Afya, biashara, kilimo, habari na TEHAMA ambazo zimekuwa na manufaa kwa vijana na nchi kwa jumla.
Haya na mengine ya maendeleo ya SUZA ni miongoni mwa matunda ya Dk. Haroun katika sekta ya elimu, hayakuishia hapo Dk. Haroun ana mchango mwengine mkubwa katika masuala ya siasa yanayoingiliana na masuala ya elimu.
Kwa mfano, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Zanzibar ilizuiwa kupata misaada ambapo kutokana na ushawishi wake yalifanyika mazungumzo na wafadhali kama vile Benki ya Dunia, mashirika kama vile USAID na SIDA na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
‘’Hatimaye misaada ilirejeshwa katika sekta ya elimu na skuli za ghorofa kujengwa unguja na Pemba’’, ilieleza taarifa ya wasifu wake.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 alikuwa ni miongoni mwa wajumbe watano wa Baraza la Mapinduzi waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk. Haroun anatambulika kwa kuwa muasisi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) ambacho awali kiliakiwa kuwa Chuo Cha Ufundi lakini kutokana na ushawishi wake kikawa Chuo Kikuu. Aidha, alitoa mchango mkubwa wa kuanzishwa Chuo kikuu cha SUMAIT wakati huo kilikuwa Chuo cha Elimu- College of Eduation.
Mnamo mwaka 2004 alitunukiwa Medali ya Heshima ya Mapinduzi na mwaka 2006 alisimamia utayarishaji wa Sera na baadaye kutungwa Sera ya Elimu. Aidha, aliandika machapisho kadhaa yaliyokuwa yakizungumzia kuhusu maendeleo na changamoto za elimu nchini.
Dk. Haroun Ali Suleiman, alizaliwa tarehe 24 Julai, 1953, katika mtaa wa Kiongoni, Kijiji cha Makunduchi, Mkoa wa Kusini, Unguja. na ni mzaliwa wa sita kati ya familia ya watoto nane.