Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Hashim Hamza Chande, amesema ushirikiano baina ya SUZA, Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Chuo Kikuu cha Cagliari cha Italia umekuja wakati muafaka hasa ikizingatiwa kuwa Chuo kinatarajia kutekeleza mradi wa upanuzi wake hivi karibuni.
Akizungumza katika kikao cha pamoja cha maofisa wa ZAWA na wa Chuo cha Italia hapo makao makuu ya SUZA Tunguu Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja tarehe (31/10/2024) alisema upanuzi wa Chuo utakuwa na mahitaji makubwa ya maji jambo linalopaswa kuwepo ushirikiano na ZAWA pamoja na wataalamu wengine ili kuiwezesha huduma hiyo kupatikana kwa ufanisi.
‘’Kama hatutawashirikisha ZAWA katika jambo hili tutakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma hii’’, alisema.
Aidha, aliongeza kuwa huu ni mradi muhimu kwa visiwa vya Unguja na Pemba ambavyo vinatumia kwa kiwango kikubwa cha maji ya ardhini.
Naye, Prof. Mshiriki wa Chuo kikuu cha Cagliari cha Italia, Dk Stefania Da Pelo alisema wamezungumza sana kuhusu kuunga mkonona kubadilishana uzoefu katika masuala ya upatikanaji wa maji Zanzibar.
Aliongeza kuwa kuna fursa nyingi za kubadilishana uzoefu na wanafunzi wa vyuo hivyo viwili.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa ZAWA, Dk. Salha Khamis Mohammed alisema ameridhishwa kwa kuanzishwa ushirikiano huu ambao utachangia kufanyika tafiti na kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa maji Zanzibar.
Aliongeza kuwa wakati umefika kutambua kiwango cha maji kinachopatikana katika ardhi Unguja na Pemba, ubora wake, wapi yameanzia na njia gani yanaelekea.
Naye, Dk. Abdallah Ibrahim, Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA amesema Italia ni nchi ambayo imeendelea na ina uzoefu mkubwa katika teknolojia na masuala ya maji.
Aliongeza kuwa kutokana na ushirikiano uliopo, SUZA na ZAWA zitafaidika hasa katika kujengewa uwezo na taaluma.
‘’ Sisi tutajifunza kutoka kwao ili kukabiliana na kasi ya ongezeko laidadi ya watu, na mabadiliko ya tabia nchi, tusipofanya jambo leo tutakabiliwa na changamoto kesho (miaka 50 ijayo)’’, alisisitiza.
Aidha, mazungumzo hayo yatafuatiwa na utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano baina ya vyuo hivi viwili.
Vyuo vikuu vya Cagliari Italia na SUZA cha Zanzibar vinashirikiana katika tafiti mbali mbali zinazohusiana na maji huku wakishirikiana na Wizara inayosimamia ustawi wa upatikanaji majichini ya Mamlaka ya ZAWA.