The State University Of Zanzibar

SUZA yazindua  maktaba ya kimtandao

MKUU wa  Chuo  Kikuu cha Taifa cha Zanzibar  (SUZA) Prof. Moh’d Makame Haji amezindua mfumo mpya wa masomo ya kimtandao  ‘Myloft – My Library  of Finger Print’  ambao utasaidia  upatikanaji wa taarifa za kimasomo   kwa njia rahisi.

Alisema mfumo huo utachangia kuwawezesha wanafunzi na wafanyakazi kufanya kazi zao  hasa ikizingatiwa kuwa kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na SUZA kila mwaka.

Akizungumza kwa niaba ya makamo Mkuu wa  Chuo,  Mkurugenzi wa Shahada za Awali SUZA, Dk. Khamis Salum aliwahimiza  wanafunzi wa Chuo hiki  kuutumia mfumo huo kujiongezea maarifa ya kielimu kwa njia ya mtandao.

Naye Mkurugenzi wa Maktaba SUZA, Bw. Moh’d Khamis Kombo alisema umefika wakati wa kutumia teknolojia ya kukusanya taarifa za kielimu kinyume na miaka 30 iliyopita.

‘’Tumehangaika sana hadi kufikia hapoa tulipo, hatukuinunua ili iwe pambo tunaamini nyinyi ndio watumiaji wetu’’, Mkurugenzi aliwaambia wageni walioshiriki uzinduzi huo.

Alisema katika kipindi hicho hakukuwa na app ya ksuaidia kupata taarifa na badala yake vitabu kutoka maktaba ndio nyenzo muhimu zilizokuwa zikitumiwa.

‘’Zamani tulipaswa kuvifuata vitabu maktaba lakini sasa App hii inapatikana  mahala popote, iwe nyumbani, sokoni au njiani utajifunza mambo mengi kwa mujibu wa mahitaji yako ya kielimu’’, alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Naye Meneja wa Kanda ya Afrika   wa RemoteXs, Mtaalamu Sila Too, alisema  kabla ya matumizi ya mfumo huo, vitabu vingi havikuweza kusomwa seuze kuazimwa.

‘’Baada ya kuona changamoto hii tukaona  ni vyema tuandae  programu hii inayotumiwa bila internet’’, alieleza

Aidha aliongeza kuwa mfumo huu nimashuhuru katika vyuo vikuu vingi vya Afrika ikiwa ni  pamoja na Kenya (133), Uganda (33), Ghana(52) na vyengine ni Zambia na Malawi na Botswana na sasa  Tanzania ambayo fursa hii inatumika kwa wingi katika vyuo vikuu kadhaa.

Alisisitiza kuwa mfumo huu unatumiwa na vyuo kuongeza maudhui yake  lakini pia kwa wenye vitabu wanaotaka visomwe mtandaoni pia huduma hii inaweza kuingizwa.

Aliwakumbusha wanafunzi na wafanyakazi kuwa  teknolojia hii inalipiwa gharama kubwa na vyuo vinavyotumiwa hivyo si busara kuwepo bila ya kutumiwa na wanafunzi na hata wafanyakazi wa SUZA kwa matumizi ya kielimu.