The State University Of Zanzibar

Kongamano la elimu bila Malipo – SUZA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Raisi, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman, amewahimiza walimu kuzingatia uzalendo, uadilifu, na utii katika kazi zao ili kuboresha sekta ya elimu Zanzibar.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Kitaaluma la kuadhimisha Miaka 60 ya Elimu Bila Malipo lililofanyika Maruhubi, Mkoa wa Mjini Unguja, Mhe. Haroun amesisitiza umuhimu wa walimu kuzingatia maadili ili kuleta matokeo bora kwa wanafunzi na taifa kwa ujumla.

Aidha. Mhe. Suleiman pia ameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzisaidia Taasisi za Elimu ya Juu kwa kuwawezesha kufanya tafiti zenye tija zitakazochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, Akimkaribisha Mgeni Rasmi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane chini ya ya Uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu na kudumisha sera ya Elimu Bila Malipo kwani imeleta mafanikio makubwa kwa taifa.

Mapema Makamu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Makame Haji, amesema Kongamano hilo linatoa fursa ya kutathmini mafanikio ya elimu kwa kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, huku akibainisha kuwa SUZA ni moja ya matunda makubwa ya juhudi hizo.

Kongamano hilo la Kitaaluma limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar lenye kauli mbiu ” Miaka 60 ya Elimu bila Malipo: Elimu, Michezo na Afya Zimeimarika.

Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano na Masoko(SUZA)