The State University Of Zanzibar

Kiswahili chaipaisha SUZA kimataifa

Na Mwandishi Wetu, SUZA

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa  Taasisi ya Taaluma ya Asia- Magharibi na Afrika ya China Prof.  Wang Xiaoming amesema wanafurahia umashuhuri Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar  (SUZA)  kutokana na mipango yake madhubuti ya uendeshaji na uzalishaji wataalamu wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kilichofanyika huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja   baina ya SUZA na taasisi anayoiongoza,  kilichowashirikisha wataalamu kutoka SUZA na ujumbe  aliouongoza katika ziara hiyo, Prof Wang alisema SUZA inatambulika  kutokana na wanafunzi wengi kupitia hapa kujifunza lugha ya Kiswahili na taaluma nyengine.

Aliongeza kuwa mnamo mwaka 2013 Vyuo hivyo vilisaini mkataba wa makubaliano ambapo matarajio yao ni kuwa na uhusiano mwema na kushirikiana katika nyanja mbali  za kitaaluma lakini pia walifanikiwa kuwaleta wanafunzi  saba (7) kuja kujifunza lugha ya Kiswahili mwaka 2015 hado 2017.

Aidha, aliongeza kuanzia mwaka 196 1 walianza kufundisha Lugha ya Kiswahili ikiwa ni taasisi  ya mwanzo  nchini humo na hivi sasa kuna lugha 20 za kiafrika zinazofundishwa huku lugha nyengine 101 rasmi  katika nchi mbali mbali pia zinafundishwa.

‘’ Tuna wanafunzi zaidi ya 1000 waliopata mafunzo ambao wanashiriki katika kazi zinazohusiana na lugha za kimataifa, wamezalisha pia mabalozi wa Umoja wa wanafunzi 5000 katika nyanja ya lugha.

Alifahamisha kuwa Tanzania na China ni marafiki wa kweli tangu miaka ya 50 ambapo wanapofikiria nchi za Afrika kwanza wanaiangalia Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Aidha, kiongozi huyo ambaye ni mkuu wa msafara wa wajumbe sita (6) alioongozana nao  ametoa fursa kwa  SUZA kuzungumza na wanafunzi wa skuli zao kuhusu ushirikiano wa kiuchumi baina ya China na Tanzania  pa amewakaribisha wanafunzi wanaopendelea kujifunza Kichina kuzuru  nchi yao na wanafunzi  wa China  kuja Zanzibar kujifunza Kiswahili.

Naye Naibu Makamo Mkuu wa SUZA  masuala ya  Mipango  Fedha na Utawala,  Dk. Hashim  Hamza Chande  alisema  Fedha Zanzibar amesema  SUZA  imekuwa ikipata mafanikio makubwa kwa uhusiano uliokuwepo ambao unahitaji Zaidi kudumishwa kwa kuangalia maeneo mengine ya kitaaluma.

‘’ Tuna darasa la Kichina (Confucious Class) na tuna wazungumzaji mahiri wa lugha hii, tunashukuru kupata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wenu  hali itakayochangia kutanua wigo wa uhusiano   uliokuwepo’’, alikumbusha.

Mapema,   Bi. Shani Suleiman Khalfan, Mkuu wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni alisema, wamekuwa wakiwasiliana na wataalamu wenzao wa China kwa lengo la kuimarisha program za ufundishaji wa lugha  nyengine.

Katika kikao, hicho wajumbe wamekubaliana kuupitia tena mkataba wa makubaliano  sambamba  na  kuziba pengo la kutokuwepo walimu wazawa wanaofundisha lugha ya Kichina nchini humo huku walimu wengine kutoka  Kenya na Ruanda wakiitumia vyema fursa hiyo.

mwisho.