Skip to main content

The State University Of Zanzibar

Mashirikano ya SUZA,HALOTEL Yatoa Tumaini Jipya kwa Wanafunzi

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimetoa shukrani kwa Kampuni ya Simu ya Mtandao wa Halotel kwa ufadhili wa Shilingi Milioni 26 uliowanufaisha wanafunzi 24 wa chuo hicho, katika zoezi la kutambua na kuthamini mchango wa kampuni hiyo katika kuwawezesha wanafunzi wenye uhitaji.

Akizungumza katika hafla ya kutoa shukurani kwa kampuni hiyo Mkurugenzi wa Shahada za Awali SUZA, Dkt. Khamis Othman, iliyofanyika tarehe 19/08/2026 katika Makao Makuu ya SUZA, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja,

Amesema mchango huo ni sehemu ya ushirikiano muhimu kati ya SUZA na wadau katika kusaidia wanafunzi kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri safari yao ya elimu.
Dkt. Khamis amesema ufadhili huo umekuwa na mchango mkubwa kwa wanufaika huku akieleza kuwa ushirikiano wa aina hiyo unaonesha umuhimu wa wadau kushirikiana na taasisi za elimu katika kutatua changamoto za vijana

Ameendelea kuwataka wanafunzi walionufaika kuthamini fursa hiyo kwa kuongeza bidii katika masomo yao na kutumia elimu wanayoipata kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha, amezihimiza taasisi na kampuni nyingine kuendelea kushirikiana na SUZA katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali, akisema mchango wa wadau una nafasi kubwa katika kuimarisha mazingira ya elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ustawi wa Wanafunzi SUZA, Salha Khalfan Khamis , amesema Halotel imekuwa mshirika muhimu wa SUZA katika kusaidia wanafunzi pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa jamii.
Amesema Ofisi ya Ustawi wa Wanafunzi itaendelea kusimamia misaada inayotolewa na wadau kwa kuhakikisha inawafikia walengwa kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na kutokuwepo kwa upendeleo.

Naye Mkurugenzi wa Halotel Zanzibar, Ngamwela Daniel Mkalimoto, amesema kampuni hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na SUZA, hususan katika kusaidia wanafunzi na shughuli zinazolenga kuleta manufaa kwa jamii.
Amesema Halotel inaendelea kutambua umuhimu wa kushirikiana na taasisi za elimu katika kuchangia maendeleo ya vijana na jamii.

Nao wanufaika wa ufadhili huo wameishukuru Halotel kwa msaada walioupata, wakisema umewasaidia kuendelea na masomo yao, huku wakiahidi kuongeza bidii katika masomo na kutumia vyema fursa hiyo