Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA YAWEKA HISTORIA TUZO ZA WATAFITI

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) – Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdalla, amesema SUZA imepata mafanikio makubwa katika utafiti, ubunifu, programu mpya za kitaaluma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Prof. Abdi Talib aliyasema hayo wakati akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda, alipotembelea banda la SUZA katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika viwanja vya Shule ya Usagara, jijini Tanga.

Akizungumza na Waziri Mkenda wakati wa ziara hiyo, Prof. Abdi Talib alisema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni SUZA kushiriki kwa mara ya kwanza katika Tuzo za Watafiti Waliochapisha Matokeo ya Tafiti Zao katika Majarida yenye Hadhi ya Juu Kimataifa, zinazotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST).

Alisema SUZA imefanikiwa kupata tuzo hiyo kupitia Mhandisi Dkt. Abdulrahim Haroun Ali Suleiman, Mhadhiri Mwandamizi (Senior Lecturer) wa SUZA, ambaye ameiwezesha Taasisi hiyo kuweka historia katika ushiriki wake wa kwanza katika tuzo hizo.

Prof. Abdi Talib amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi zinazoendelea kufanywa na SUZA katika kuimarisha utafiti, kuongeza uchapishaji wa matokeo ya tafiti katika majarida ya kimataifa yenye hadhi ya juu, pamoja na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa na watafiti wa Chuo yanatoa mchango katika kutatua changamoto na kuleta maendeleo katika jamii.

Prof. Abdi Talib pia alieleza kuwa ushiriki wa SUZA katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu programu mpya za kitaaluma zinazotolewa na Chuo, zikiwemo Shahada ya Kwanza ya Akili Unde na Sayansi ya Data (Bachelor of Artificial Intelligence and Data Science) pamoja na Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Usafirishaji na Uendeshaji wa Bandari (Bachelor of Shipping and Port Logistics Management).

Katika eneo la ubunifu, alisema SUZA imewasilisha bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, zikiwemo mfumo wa uuzaji wa samaki kwa njia ya mtandao, mfumo wa uchimbaji unaosaidia kugundua changamoto zinazoweza kujitokeza chini ya ardhi, mfumo wa ufuatiliaji wa afya (Health Monitoring System), pamoja na bunifu mbalimbali zinazohusiana na ujasiriamali.

Akizungumzia maendeleo ya miundombinu, Prof. Abdi Talib alisema SUZA inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, kuimarisha utafiti na ubunifu, pamoja na kuboresha huduma kwa wanafunzi.

Ushiriki wa SUZA katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu unaendelea kutoa fursa kwa Chuo kuonesha mchango wake katika maendeleo ya elimu ya juu, utafiti na ubunifu, sambamba na uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya Taifa na fursa zinazotokana na uchumi wa buluu.