The State University Of Zanzibar

SUZA, UNICAM na Bremen washirikiana kitaaluma

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) Prof. Salum Seif Salum amesema SUZA imepata fursa ya kujiimarisha kitaaluma kupitia ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Camerino cha Italia na Bremen cha Ujerumani.

Hayo ameyasema kwenye mkutano na washirika hao ukiwashirikisha pia wakuu wa Skuli za SUZA na wanafunzi uliofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Utalii Maruhubi tarehe 14/01/2026, alisema ushirikiano huo utawezesha kuimarisha tafiti zake katika masuala ya afya, kilimo, elimu na akili mnemba.

Katika mkutano huo, washiriki kutoka Vyuo vikuu waliwasilisha tafiti kuhusiana na masuala mbali mbali yanayohusu Zanzibar miongoni mwao zikiwa zimefanywa na wanafunzi wazawa walipokuwa wakiendelea na masomo yao katika vyuo hivyo huko nje.

Prof. Salum alifahamisha kuwa SUZA inalenga kuanzisha kozi mpya za akili mnemba ambazo zinahitaji tafiti ili kutoa wepesi wa kuanzishwa kwa program hizo hivyo mashirikiano hayo yameleta taswira mpya ya mashirikiano katika sekta hiyo muhimu duniani

Kwa upande wake Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba Dk. Salma Abdi Mahmoud, amesema ujio huo umetoa fursa ya ushirikiano ikiwemo kubadlishana wataalamu, wanafunzi na kufanya tafiti za kisayansi, kilimo na fani nyengine zinazotolewa na SUZA, ambapo itasaidia kukuza uelewa zaidi katika maeneo hayo

Dk. Salma ambae pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na kizazi alieleza kutokana na upungufu wa tafiti za kilimo, SUZA inaangalia namna ya kushirikiana na wataalamu hao ili kutoa mchango wao kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Camerino (UNICAM) Prof. EmanueleTondi ameeleza kuwa chuo chake kinathamini ushirikiano huo na kinaahidi kufanya kazi kwa karibu na taasisi za SUZA.

Mkutano huo wa siku mbili utatoa mwelekeo wa SUZA katika vipengele vya ushirikiano baada ya kujadili baada ya mawasilisho ya mada mbali mbali ziliztolewa na wadau na wazawa.