






Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimepokea ujumbe wa maofisa kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) tarehe 8 Januari 2026 katika makao makuu yake Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja. Ziara hiyo ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya TANAPA na wadau wake, sambamba na ushiriki wao katika maonesho ya biashara yanayoendelea Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume, Prof. Moh’d Makame Haji alieleza kuwa Zanzibar na Tanzania Bara zina fursa nyingi za kuendeleza utalii wa ndani. Alisisitiza kuwa utalii wa ndani haujapewa kipaumbele ipasavyo licha ya jitihada kubwa zinazochukuliwa katika kuhifadhi historia na urithi wa kale. Kupitia Kigoda cha Karume, SUZA imefanikiwa kukusanya kumbukumbu kwa njia ya maandiko, video na picha ili kuwajenga vijana kitaaluma na kuwapa mbinu za uongozi bora. Prof. Haji aliongeza kuwa Kigoda cha Karume kina jukumu la kuendeleza elimu kwa kufanya tafiti, kuandaa makongamano na kuchapisha majarida yanayohifadhi urithi wa Hayati Mzee Abeid Amani Karume kwa faida ya Taifa na vizazi vijavyo.
Naye Bi. Amina Salum kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha alieleza kuwa TANAPA inamiliki hifadhi 21 zenye historia tajiri, ikiwemo maeneo yaliyotumika na viongozi wa kijadi kujificha wakati wa vita. Aliongeza kuwa utalii wa ndani ni muhimu kwa wanafunzi na wananchi kwani unawapa nafasi ya kujifunza na kutoa huduma bora kwa wageni.
Kwa upande wake, Geofrey Kyando kutoka Hifadhi ya Mkomazi alisema TANAPA inatarajia wadau wake kuandika maoni yatakayotumika kuimarisha huduma zake. Aliongeza kuwa ushirikiano na SUZA unaweza kuendeleza uwekezaji katika sekta ya utalii wa ndani, ikiwemo ujenzi wa nyumba za wageni za muda mfupi na ulishaji wa vyakula vya asili.
Aidha, mazungumzo hayo ya mashirikiano kupitia Kigoda cha Karume yameainisha maeneo mapana ya ushirikiano kati ya SUZA na TANAPA. Mashirikiano haya yanahusisha tafiti na uendelezaji wa hifadhi za kihistoria, kukuza utalii wa ndani na biashara, kuimarisha tafiti za lugha na utamaduni, pamoja na kutumia TEHAMA kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu na kutangaza vivutio vya utalii. Pia, mashirikiano haya yanalenga kuimarisha elimu na utafiti wa kijamii kwa kuandaa makongamano, tafiti na machapisho yanayohusiana na historia, utalii na maendeleo ya kijamii kwa faida ya Taifa na kizazi kijacho.
Kwa upande wake Dkt. Mussa A. Makame, Afisa Utawala na Mtendaji wa Kigoda cha Karume ameushukuru uongozi wa TANAPA kuandaa ziara hiyo na kusema kuwa TANAPA imefungua ukurasa mpya wa mashirikiano kati ya taasisi hizi mbili. Kupitia Kigoda cha Karume, SUZA na TANAPA wana nafasi ya kuimarisha utalii wa ndani, kuhifadhi historia na kuendeleza ujuzi wa vijana. Ushirikiano huu unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa Taifa hususani katika kukuza ajira, ujasiriamali, TEHAMA na utamaduni wa Tanzania.