The State University Of Zanzibar

Michezo TUSA yaing’arisha SUZA

Time ya Michezo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) imewasilisha nyumbani vikombe sita (6) na medali nane (8) kufuatia ushindi wa mashindano ya michezo iliyovishirikisha Vyuo Vikuu vya Tanzania (TUSA).
Michezo iliyoshindaniwa ni WoodBall (mshindi wa kwanza wanaume na mshindi wa pili wanawake), Chess (mshindi wa kwanza wanawake), Scrabble (mshindi wa kwanza wanaume na pia wanawake) na Tabletenis.
Katika michezo hiyo wanamichezo hao walijizolea medali nane (8) zikiwemo mbili (2) za dhahabu na na sita (6) za Silver kwenye michezo mbali mbali.
Kaimu Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Abdi Talib Abdalla alisema SUZA inaona fahari kwa kupata ushindi huo mkubwa ambao unaonesha kuwa wana SUZA hawakwenda kushiriki lakini walikwenda kushindana.
‘’ Nilijua mtashinda lakini sikujua kama mtashinda namna hii’’, alisema Prof. Abdalla.
Aidha aliwaahidi wanamichezo hao kuwa atahakikisha kuwa michezo itazidi kuipaisha SUZA na kwamba hawezi kuiacha michezo ikidorora wakati yeye akiwepo SUZA.
Aliongeza kuwa, katika kuleta ufanisi wa michezo, SUZA haitakuwa na kipingamizi endapo mashindano hayo yatafanyika nje ya Tanzania.
‘’ Mimi mwanamichezo siwezi kuona katika wakati wangu michezo inaanguka’’, alieleza Prof. Abdalla.
Prof. Abdalla aliwatanabahisha wanafunzi umuhimu wa kushiriki kwenye michezo ikiwa ni pamoja na kujifunza kushirikiana, kuchangamsha mwili na kujijengea uwezo wa kufikiri.
Mratibu wa Michezo wa SUZA, Bw. Hassan Khairalla alisema ushindi huo umeleta heshima kwa SUZA na kuwatia ari wanamichezo wake kutaka kuongeza idadi ya michezo watakayoshiriki katika mashindano yajayo.
Aidha, aliongeza kuwa SUZA imeandaa Sera ya Michezo ili kutoa fursa kwa wanafunzi kushiriki kwa kujiamini na kutatua changamoto zinazowakabili huku wakiendelea na masomo yao.
Nae Mlezi wa wanafunzi , Bi Salha Ramadhan, aliishukuru SUZA kwa kuwawezesha kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa.
Naye Mwenyekiti wa Sera ya Michezo ya SUZA, Dkt. Ali Adnan Idarous alisema SUZA inaona fahari kwa ushindi huu na kutoa wito kuandaliwa mazingira yatakayoiwezesha Sera hiyo kuanza kutumika haraka iwezekanavyo.
Aidha, Waziri wa Michezo wa serikali ya Wanafunzi ya SUZA, Bw. Shiblian Mo’hd amependekeza kuwa SUZA iongeze ushiriki katika michezo mingine, wazingatiwe muda wao wa masomo na ushiriki wao katika michezo ili kuepukana na changamoto katika taaluma.