






SUZA imeonesha utayari wake wa kuendeleza ushirikiano wa karibu na Chuo Kikuu cha SAN cha Poland, ikiwa ni pamoja na kukiomba Chuo Kikuu cha SAN kafungua tawi lake SUZA, kutoa fursa za kuwajengea uwezo wanataaluma katika mafuala ya tafiti na kubadilishana uzoefu katika ufundishaji. Hatua hii inalenga kuimarisha mahusiano ya kielimu kati ya vyuo hivyo viwili na kupanua fursa za kitaaluma kwa wanafunzi na walimu kutoka pande zote.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Makamu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala SUZA, Dkt. Hashim Hamza Chande, alipokutana na Mkurugenzi wa Mahusiano na Miradi ya Kimataifa kutoka SAN University ya Poland, Bi Aleksandra Zayac, katika makao makuu ya SUZA, Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Tunaamini miradi kama ya European Union Staff and Students Mobility – Erasmus+ itaendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kitaaluma baina ya walimu na wanafunzi kutoka vyuo vyetu viwili. Akiendelea kufafanua, Dkt.Hashim Hamza Chande alibainisha kuwa SAN University ina nafasi kubwa ya kufungua kampasi hapa Zanzibar, hatua ambayo itafungua milango kwa wanafunzi kutoka nchi jirani kama Kenya, Uganda, Nigeria, na nyinginezo, kushiriki masomo ya juu bila kuhitaji kusafiri mbali. Alitoa mfano wa mafanikio ya chuo cha India cha Teknolojia kilichopo Zanzibar, ambacho kimekuwa mkombozi kwa wanafunzi wasioweza kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya elimu.
Kwa upande wake, Bi Aleksandra Zayac alieleza kuwa SAN University inathamini sana ushirikiano wa kimataifa, na kupitia programu ya Erasmus+, wako tayari kushirikiana kwa karibu na SUZA – hasa kupitia Skuli ya Biashara, ambayo inaendana na kozi zinazotolewa na chuo chao.
“Tunaona uwezekano mkubwa wa kushirikiana na SUZA si tu katika Skuli ya Biashara, bali pia katika Skuli nyingine kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kitaaluma na kubadilishana uzoefu wa kielimu,” aliongeza Bi Zayac.
Ushirikiano huu unaotarajiwa kati ya SUZA na SAN University unaonyesha mwamko mpya wa kimataifa katika sekta ya elimu ya juu Zanzibar, huku ukilenga kuimarisha ubora wa elimu, utafiti, na ubadilishanaji wa maarifa kwa manufaa ya jamii nzima. Pia aliendelea kuelezea kuwa ushirikiano huo utaiwezesha SUZA kupata miradi ya tafiti ya kinataifa kupitia Horizon europe na kuwapatia mafunzo na nyezo za utafiti wanataaluma wa SUZA.