The State University Of Zanzibar

Kiswahili Chazidi Kuunganisha Dunia: SUZA na Osaka Waanza Safari ya Elimu ya Pamoja

Chuo Kikuu cha Osaka, Japani, kimefungua fursa mpya za kitaaluma kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kwa kusaidia wanafunzi na wataalamu wake kujiunga na taasisi mbalimbali za kimataifa zinazotoa programu za masomo ya Sayansi na lugha.

Akizungumza katika kikao maalum cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kati ya SUZA na Chuo Kikuu cha Osaka, Msaidizi Mkuu wa Chuo cha Osaka, Mwalimu Bi. Jamila, alisema chuo hicho kina vitivo 11 vinavyoongoza katika fani za Sayansi na taaluma nyinginezo, na kwamba kipo tayari kusaidia kuanzishwa kwa mikataba mingine ya ushirikiano wa kielimu.

“Sisi tuko tayari kuwasaidia kujiunga na vyuo vingine kwa kuandaa mikataba zaidi ya ushirikiano,” alisema Mwalimu Bi. Jamila
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Prof. Moh’d Makame Haji, alieleza kuwa lugha ya Kiswahili imekuwa kiungo kikubwa katika kuanzisha ushirikiano huu. Alisema kuwa Osaka walikuwa wakitafuta chuo kinachofundisha Kiswahili kama lugha ya asili, hali iliyowapelekea kushirikiana na SUZA.

Tuliona Kiswahili kitatuwezesha kushirikiana. Tusingeweza kushirikiana nanyi kama hakukuwa na msingi wa kitaaluma. Osaka walikuwa wanatafuta chuo kinachofundisha Kiswahili, lugha ambayo inaendelea kukua kwa kasi duniani,” alieleza Prof. Moh’d Makame Haji.

Katika mkataba wao ulioanzishwa mwezi Julai mwaka huu, wakati wa ziara ya SUZA nchini Japani kushiriki maonesho ya kielimu, vyuo hivyo vilikubaliana kubadilishana wataalamu na wanafunzi wanaofundisha lugha za Kiswahili na Kikorea, pamoja na kushirikiana katika tafiti. Utekelezaji wa makubaliano haya unatarajiwa kuanza mara baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.

Katika hatua nyingine, Mwalimu Bi. Jamila alibainisha kuwa wanafunzi wa ngazi ya Uzamili na Uzamivu kutoka Japani wako tayari kuja Zanzibar kujifunza Kiswahili na kufanya utalii wa kielimu, hata kwa gharama zao binafsi. Alisema kuwa wanafunzi hao wana uwezo mkubwa wa kuwafundisha wanafunzi wa Japani na hivyo kuboresha uelewa wa lugha ya Kiswahili nchini humo.

Kumiko Miazaki, kutoka Idara ya Kiswahili ya Osaka, alieleza nia yake ya kufanya utafiti wa lahaja mbalimbali za Kiswahili, ikiwemo lahaja ya Kiunguja katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, na lahaja ya Kipemba katika mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba. Aliongeza kuwa video ya SUZA iliyooneshwa katika maonesho ya Japani ilipokelewa kwa pongezi na ilivutia watu wengi kutokana na ubunifu wa mbinu za ufundishaji wa Kiswahili.

Kwa upande mwingine, Dkt. Ali Kassim Yussuf, Mkuu wa Idara ya Lugha za Kigeni, alielezea ongezeko la hamasa kwa Wajapani kujifunza Kiswahili. Alipendekeza matumizi ya teknolojia ya kisasa kama vile akili mnemba (machine learning) na akili bandia (AI) ili kurahisisha usambazaji wa maarifa kwa pande zote mbili – jambo ambalo liliungwa mkono na ujumbe kutoka Osaka.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu mbalimbali wa SUZA akiwemo Bi. Shani Suleiman Khalfan, Mkuu wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni; Bi. Fatma Soud Nassor, Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Taaluma za Kiswahili na Uenezi; Dkt. Abubakar Makame Fakih, Mkuu wa Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni; Dkt. Kijakazi Omar Makame, Mkuu wa Idara ya Kiswahili; Dkt. Mtaib Abdulla Othman, Mkuu wa Idara ya Sheria; pamoja na Dkt. Ally Kassim Yussuf, Mkuu wa Idara ya Lugha za Kigeni.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 26 Agosti 2025 katika Makao Makuu ya SUZA, Tunguu – Mkoa wa Kusini Unguja.

.