The State University Of Zanzibar

SUZA Yajipanga Kuinua Elimu ya Bahari

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kinapanga kuanzisha taasisi ya ubaharia kama sehemu ya juhudi zake za kupanua mafunzo ya kiufundi na kitaaluma visiwani Zanzibar. Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Moh’d Makame Haji, alipokutana na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, katika makao makuu ya Tunguu mapema leo asubuh.

Katika mazungumzo yao, Prof. Moh’d Makame Haji alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Indonesia ni wa muda mrefu, ulioasisiwa na viongozi waasisi wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.

“Sisi ni marafiki wa karibu sana. Kihistoria, kulikuwepo na ushirikiano mzuri baina ya nchi hizi mbili, na tumekuwa pamoja kwa karne nyingi,” alisema Prof. Moh’d Makame Haji.

Aidha, alisifu juhudi za viongozi wa sasa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kufungua milango ya kidiplomasia, ikiwemo kufunguliwa kwa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia.

Prof. Moh’d Makame Haji alieleza kuwa viongozi hao wawili wapo mstari wa mbele katika kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta mbalimbali, zikiwemo elimu, afya, na kilimo.

Kwa upande wake, Balozi wa Indonesia, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, alieleza kuwa Indonesia ina fursa nyingi za elimu na tayari imetoa nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Tanzania. Hata hivyo, alieleza kuwa bado idadi ya waombaji kutoka Zanzibar ni ndogo na kuwahimiza Wazanzibari kuchangamkia fursa hizo kwa wingi.

Balozi Jatmiko alitaja fursa nyingine za ushirikiano kuwa ni pamoja na kushirikiana kupitia mtandao (online) katika nyanja za kilimo, afya, mwani, na karafuu, ili kuongeza maarifa na ujuzi wa wataalamu wa kutoka suza kupitia mijadala ya kitaalamu. Huku akisisitiza kuanzishwa kwa madarasa ya lugha ya Kiindonesia (Bahasa Indonesia) ambayo yataendeshwa Zanzibar kwa ufadhili kamili wa Serikali ya Indonesia.

Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili pamoja na maafisa kutoka pande zote mbili yamefungua milango ya maandalizi ya hati ya makubaliano rasmi (MoU). Balozi huyo alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kushindwa kutekeleza makubaliano hayo, kwa kuwa mazingira ya ushirikiano tayari yapo.