The State University Of Zanzibar

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar wakagua maendeleo ya ujenzi wa ukuta wa Kampasi ya Benjamin William Mkapa

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar wakagua maendeleo ya ujenzi wa ukuta wa Kampasi ya Benjamin William Mkapa iliyopo Mchangamdogo, Wilaya ya Wete Kisiwani Pemba.
Akikagua ujenzi huo Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Moh’d Makame Haji amesema lengo la ujenzi huo ni kuangalia maendeleo ya kazi ya ujenzi inayoendelea

Prof. Haji amesisitiza kuwa ujenzi huo utaimarisha mazingira mazuri ya kampasi ya MchangaMdogo na kuongeza hifadhi ya eneo lake pamoja na kuimarisha usalama wa wanafunzi, wafanya kazi na mali za chuo na kulifanya liwe rafiki zaidi kwa kuendeleza shughuli za kitaaluma.

Aidha alitanabaisha kuwa, Chuo kinaandaa mpango mkakati kwa ajili ya kuendeleza Kampasi hiyo ili kuweza kuongeza programu mbalimbali za masomo kwa mujibu wa mahitaji ya nchi. Kwa kuanzia katika mwaka huu wa masomo 2025/2026 Chuo kwa mara ya kwanza kimeanzisha kutoa program ya Shahada ya Kwanza ya Ualimu wa Sayansi katika Kampasi hiyo.

Nae Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Hashim Hamza Chande amesema kuwa, ujenzi huo wa ukuta unaoendelea wa mita 400 utagharimu kiasi cha shilingi milioni mia moja na themanini na unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2025 kwa awamu hii ya kwanza.

Àidha alieleza kuwa, Chuo pia kimetenga milioni 400 katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo wa ukuta wa eneo lililobaki la mita 529. Ukaguzi huo wa ujenzi umefanyika leo tarehe 24 Julai, 2025.