






Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimesaini HAti ya Mashirikiano na Taasisi ya African Peer Review Mechanism (APRM)-Tanzania. Mkataba huo umesainiwa na Profesa Mohd Makame Haji, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa upande wa SUZA na Ndg. Lamau August Mpolo, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya APRM Tanzania katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) uliopo Tunguu, Zanzibar tarehe 23 Julai, 2023.
Baada ya kutoa shukurani zake za dhati kwa uongozi wa APRM-Tanzania, Makamu Mkuu wa SUZA amesema utiaji saini wa Mkataba huo umefungua milango ya mashirikiano yanayojikita katika kuchochea ustawi wa jamii, utawala bora, demokrasia na maendeleo kwa ajili ya maslahi ya Taifa na wananchi wake wote kwa ujumla. Aidha, amesema kuwa Mkataba huo wa Mashirikiano unaziwezesha Taasisi hizo mbili kufanya kazi kwa kwa pamoja katika maeneo ya utafiti, kazi za kitaaluma, machapisho ya pamoja, miradi ya kimaendeleo na kazi za ushauri elekezi.
Sambamba na hayo, Makamu Mkuu wa Chuo alitoa pongezi zake za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kwa jitihada zao madhubuti wanazozichukua katika kukuza ustawi na maendeleo ya wananchi wa Tanzania. Pia, aliongeza kuwa hatua ya utiaji saini Mkataba wa Mashirikiano ni miongoni mwa shughuli za uungaji mkono jitihada na maelekezo wanayoyatoa kwa watendaji na wasimamizi wa Taasisi za umma na mashirika mbalimbali nchini juu ya uandaaji wa mikakati ya kuchochea mabadiliko na kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla na kufikiwa malengo ya dira 2050.
‘’ Ushiriki wa taasisi hizi ni muhimu katika kutimiza shabaha zilizowekwa kufikia dira hiyo’’, alisisitiza Prof. Haji.
Prof. Haji aliiambia APRM kuwa SUZA iko tayari kushirikiana nao katika tafiti mbali mbali kwa kufanya tafiti zitakazosaidia kutengeneza na kukwamua changamoto zinazojitokeza zinaendana na mahitaji ili kufikia mipango mikuu ya serikali iliyowekwa.
Alifahamisha kuwa kuwepo kwa SUZA ni mchango mkubwa wa kitaalamu na uwezo walionao kusaidia maendeleo ya utekelezaji wa shughuli zake wanazozifanya za ndani na nje ya Tanzania.
‘’Tafiti zinazofanyika ni lazima ziangalie mahitaji halisi ya jamii, soko la ajira na kumtizama mwananchi wa kawaida kuhakikisha ananufaika’’, alisisitiza Prof. Haji.
Nae Ndg. Lamau August Mpolo, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya APRM-Tanzania ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa kuwapa mashirikiano katika hatua zote za maandalizi ya Mkataba huo hadi kukamilika kwake na kufikia kilele cha kutiwa saini. Pia, aliengeza kuwa Taasisi ya APRM-Tanzania ina imani kubwa na uongozi wa sasa wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar katika kusimamia na kusaidia kufanikisha shughuli za maeneo yote ya mashirikiano kwa mafanikio makubwa zaidi. Pia, alisisitiza kuwa Taasisi ya APRM-Tanzania itaendelea kushirikiana na wataalamu kutoka SUZA katika shughuli zake mbalimbali kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya Taifa la Tanzania katika nyanja zote ikiwemo nyanja ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka SUZA na Taasisi ya APRM-Tanzania. Washiriki hao ni pamoja na Dkt. Hashim Hamza Chande, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayehusika na Mipango, Fedha na Utawala, Wakuu wa Skuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara mbalimbali za SUZA na Nd. Badria Atai Masoud, Meneja wa Habari na Mawasiliano kutoka Taasisi ya APRM-Tanzania.