The State University Of Zanzibar

SUZA  kuongoza  utoaji taaluma Afrika

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Makame Haji, amesema SUZA kinaendelea kujipanga kutanua wigo ili kuwa Chuo kinachoongoza kwa kutoa taaluma bora katika nchi za kiafrika.

Akizungumza na ujumbe watu sita kutoka katika kituo cha Uchapishaji  wa Vitabu cha Qunyan cha  China kilichoko chini ya  Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal University  (ZNU) cha China katika kikao kilichofanyika  ofisi za makao makuu ya SUZA, Tunguu  Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 11/07/2025.

Alitaja miongoni mwa hatua zinazoendelea (akiashiria kuwaonesha kwa nje) ni kujenga majengo ya kisasa kwa ajili ya dakhalia ya wanafunzi, majengo mawili ya Skuli ya Kilimo na Maabara.

Aidha, alifahamisha kuwa katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Chuo hiki, SUZA imeimarisha utendaji ikiwa ni pamoja na masuala ya tafiti, ushauri wa kijamii na kufanikiwa kutatua changamoto zinazowakabili wanajamii na kuongeza programs za masomo katika ngazi mbali mbali.

‘’Kwa upande wa programu tumeimarisha utoaji elimu katika masuala yanayohusiana na afya, Sayansi, kilimo, elimu, masuala ya biashara na  lugha saba  za kimataifa zinazofundishwa kikiwemo Kichina lakini pia Kiswahili kwa wageni ‘’, alieleza, Prof. Haji.

Aliongeza kuwa hivi karibuni, SUZA imeanzisha Taasisi  inayotoa mafunzo ya bahari na kuunga mkono utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imezungukwa na bahari na matumizi ya bahari ni miongoni mwa njia zinazotegemewa kukuza uchumi na kujipatia kipato.

Naye kiongozi wa msafara huo,  ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi ya uchapishaji ya Kituo hicho,  Bw. Hui Xu,   aliyewahi kuwa Rais wa Chuo cha  ZNU amevutiwa na utekelezaji wa majukumu ya  SUZA na anatarajia kuwa uhusiano huu utazidi kuimarika hasa maeneo ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence).

Chuo cha ZNU pia kimetiliana saini mkataba wa kufundisha somo  la Kichina kuanzia mwaka 2024 na kwa sasa kuna wataalamu wanne wanaoshirikiana na wazawa kufundisha somo hili katika Kampasi ya SUZA huko Nkurumah lakini pia linafundishwa katika baadhi ya skuli za sekondari  nchini.