The State University Of Zanzibar

APRM yawafungulia fursa wanataaluma SUZA

Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Makame Haji amepokea wazo la kushirikiana na Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa Afrika Kujipima kwa Vigezo vya Utawala Bora (APRM) utakaoongeza kasi ya utekelezaji wa dhana hiyo kuwaongezea ujuzi wanataaluma kwa kushirikiana na wadau wengine katika kutoa elimu.


Hatua hiyo imefikiwa katika kikao kilichowakutanisha watendaji wa APRM na SUZA kilichofanyika makao makuu ya SUZA Tunguu mkoa wa kusini Unguja, (27/03/2025) Kilichojadili namna watakavyoweza kufanya kazi kwa pamoja.

Akizungumza katika kikao hicho Prof. Haji alisema ushirikiano wao ni fursa muhimu kwani SUZA nayo itaweza kusikika na kubadilishana uzoefu kwa kufanya kazi na taasisi nyengine.

‘’ Chuo kinaendeshwa kwa vigezo vya Kamisheni ya Vyuo Vikuu vya Tanzania (TCU) na ubora ukishuka vigezo vinakukamata na kukulazimisha kutotumia program fulani hadi urekebishe hali hiyo’’, alisema Prof. Haji.


Alieleza kuwa kumekuwa na matokeo mazuri ya utekelezaji wa majukumu ya SUZA kutoka na kufanya tathmini kila baada ya miaka mitano ambapo tathmini ya mwisho ilifanyika mwaka 2025 na Chuo kilipewa hati ya kuendelea na shughuli zake.


Aidha, aliongeza kuwa kwa vile ni Chuo cha Umma kina mamlaka kadhaa zinazofanya tathmini ikiwa ni pamoja na kamati ya ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi na pia miradi ya maendeleo ya mashirika ya kimataifa pia ina wakaguzi wake.


Naye Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usimamizi la APRM Bw. Said Ali Mussa, alisema taarifa za APRM hujadiliwa na wakuu wa nchi wa Umoja wa Afrika (AU) ambazo huangalia maendeleo yaliyofikiwa na changamoto na namna gani changamoto hizo zinazovyoweza kupatiwa suluhu.


Katibu Mtendaji wa APRM, alisema taasisi hiyo ni wakala wa AU anayeratibu mpango wa hiari wa nchi wanachama wanaojipima katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora ambapo Tanzania ilijiunga rasmi mwaka 2004.


Katika mpango huo nchi ziliona umuhimu wa kuwa na chombo ambacho kitatoa tathmini kwa nchi wanachama wa Umoja huo badala ya kuyaachia mataifa mengine kufanya kazi hiyo kwa vigezo vyao.


Akizungumza katika kikao hicho, katibu Mtendaji alipendekeza kuwa taasisi hivyo ni vyema zikawa na mahusiano ya kudumu ambayo ambapo taasisi ya APRm inaweza kuchangia kutolewa mihadhara kwenye masuala ya utawala bora kwa kuleta wataalamu kwa kushirikiana na wataaalamu wazawa

Hii ni fursa ambapo tunapotoa elimu tunalazimika kuwa na wataalamu wetu wenyewe kwa hivyo hii ni fursa ambayo itawatangaza wataalamu wa SUZA kushiriki katika kutoa mihadhara katika nchi mbali mbali’’, alisema Lamau.


Aliongeza kuwa hivi karibuni walipokea maombi ya taasisi inayohitaji wataalamu ambapo waliwatumia link itakayowawezesha kutimiza mahitaji yao.


‘’Kwenye utoaji wa elimu tutashirikiana, suala hili linahitaji wabobezi’’, alifahamisha Katibu Mtendaji.


Awali, masuala muhimu yaliyokuwa yakiangaliwa katika taasisi hii ni demokrasia na siasa, maendeleo ya uchumi kwenye sera, kanuni, namna gani inavyowajibika kwa wananchi wake, na utawala bora kwenye mashirika binafsi na baadaye kuongezwa maeneo mengine kwa mujibu wa mahitaji ya nchi wanachama.