Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dk. Hussein Mwinyi amevutiwa na ongezeko la wahitimu wanawake ambao wanaendelea kuongezeka katika programu mbali mbali zinazotolewa katika Chuo hiki.
Alisema katika mwaka wa masomo 2023/2024 wahitimu 2791 wametunukiwa Shahada mbalimbali ambao sawa ongezeko la asilimia 7.7 ikilinganishwa na idadi ya wahitimu 2101 wa mwaka jana.
‘’Nimefarijika kuona kwa mara nyengine tena tuna idadi kubwa ya wahitimu wanawake kwa asilimia 61 ikilinganishwa na idadi ya wahitimu wanaume ambao ni asilimia 39’’, alisema Dk. Mwinyi.
Alifahamisha kuwa hali hii inaleta faraja ikizingatiwa kauli isemayo ‘ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii’. Kama ilivyo kauli mbiu ya SUZA ‘kichocheo cha mabadiliko ya jamii’
Aliongeza kuwa ana matumaini wahitimu hao watakuwa sehemu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Ameridhika chuo kinaenda sambamba na mabadiliko ya mitaala kwa kuanzishwa programu nne za ualimu nazo ni Shahada ya Elimu na Michezo na Sayansi ya Michezo, Shahada ya Elimu Mjumuisho na Mahitaji Maalum, Shahada ya Elimu ya Awali na Shahada ya Lugha.
‘’ Uanzishwaji wa program hizi una tija katika sekta ya elimu na kuiwezesha Serikali kufikia malengo iliyojiwekea.’’, alisema Dk. Mwinyi.
Mapema Makamo Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji alisema SUZA imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kwa mujibu wa mikakati na mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2025, Dira ya Maendeleo 2050.
Alielezea matumaini yake kuwa SUZA itatoa elimu bora inayoendana na mahitaji ya jamii na kwenda sambamba na kauli mbiu ya kuwa SUZA ni Kichocheo cha Mabadiliko.
Aliwapongeza wahitimu wote kwa kukamilisha safari yao ya masomo na kuwakumbusha kuwa isiwe mwisho wa kujipatia elimu bali waendelee kutafuta elimu kwani elimu haina mwisho.
‘’Leo isiwe mwisho wa safari yenu ya mwisho ya elimu baki ianze’’, alisisitiza Prof. Haji alisema.
Naye Mwenyekiti wa SUZA, Bi Hamida Ahmed Mohammed, alimshukuru Dk. Mwinyi kwa kwa jitihada zake za kuimarisha Chuo katika nyanja za tafiti, taaluma na huduma.
Aidha, aliwashukuru washiriki wa maendeleo kwa msaada mkubwa wanaoutoa katika kuchangia maendeleo mablimbali ikiwa ni pamoja na elimu.
Vilevile, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumushi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu (doctor of Philosophy- Honoris Causa) kutokana utumishi wake wa muda mrefu uliotukuka.
Katika mahafali hayo, wahitimu wa fani ya uuguzi na ukunga wa Stashahada na Shahada waliapa kiapo cha uaminifu na uadilifu na wauguzi na wakunga hawakuwa miongoni waliohitimu pia waliasimamishwa kuapa kiapo hicho.
Mahafali yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita, Spika Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, wabunge na wawakilishi.