



Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, Profesa Makame Mohammed Haji, amesema Chuo hicho kinaendelea kujidhatiti katika kuandaa wanafunzi watakaoweza kujiajiri na kuajiriwa kwenye taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi pamoja na kukuza ujuzi wa vitendo, ubunifu na maarifa ya kisasa ili kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na uwezo wa kushindana kwenye soko la ajira linalobadilika kwa kasi.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wiki ya utambulisho wa wanafunzi wapya ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) 2025-2026. katika Ukumbi wa Dkt Ali Mohammed Shein Tungu Mkoa wa Kusini Unguja 17/11/25 amesema
kuwa SUZA itaendelea kutoa elimu bora yenye viwango vya kimataifa, kwa kuzingatia ustawi na maendeleo ya mwanafunzi katika nyanja zote za kitaaluma na kijamii huku akibainisha dhamira ya Chuo ni kumwandaa kijana wa kitanzania kuwa mtaalamu mwenye maadili, uadilifu na mchango chanya kwa Taifa, sambamba na kuhakikisha miundombinu na mazingira rafiki ya kujifunzia yanaimarishwa kila mwaka.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi SUZA, Profesa Abdi Talib Abdalla, amewataka wanafunzi wapya kuzingatia ushirikiano katika masomo na maisha ya Chuo, ili kufanikisha safari yao ya kielimu huku akiwaaonya dhidi ya udanganyifu wa kitaaluma pamoja na kusisitiza kuwa kosa hilo haliwezi kuvumilika katika Chuo hicho.
Aidha, amesema ofisi yake itakuwa karibu na wanafunzi, ikiwa tayari kuwasaidia katika masuala ya kitaaluma na kutoa mwongozo utakaowasaidia kutimiza malengo yao.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala wa SUZA, Dkt. Hashim Hamza Chande, amesema jumla ya wanafunzi 8,762 waliomba kujiunga na chuo, lakini waliofanikiwa kupata nafasi ni 5,176 tu kutokana na vigezo na uwezo wa Chuo katika kudhibiti ubora wa elimu pamoja na kutowa wito kwa wanafunzi hao kutumia ipasavyo fursa hiyo muhimu katika chuo pekee cha Serikali kilichopo Zanzibar.
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, SUZA, kilianzishwa mwaka 2001 kikiwa taasisi ya Elimu ya juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kikijikita katika kutoa elimu ya juu, utafiti na huduma kwa jamii. Miaka ya hivi karibuni SUZA imepanuka na kuwa miongoni mwa vyuo vinavyoongoza kwa ubora Tanzania, kikitoa fani mbalimbali kuanzia ualimu, sayansi za afya, utalii, lugha, uchumi, Biashara, Ujasiriamali, Fedha na Benki, TEHAMA, Kilimo, Kiswahili kwa watumiaji wa lugha nyingine Mifumo na maeneo mengine muhimu kwa maendeleo ya Taifa.