Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeambatana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar katika ziara maalum iliyofanywa leo tarehe 18 Novemba, 2024 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kilichopo Mkoa wa Mbeya, ili kujifunza kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET).
Ziara hii imefanyika baada ya kikao cha kamati kilichopokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa HEET SUZA kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2024 na 2024/2025 kilichofanyika SUZA tarehe 8 Novemba, 2024.
Lengo kuu la ziara hii lilikuwa kujifunza na kubaini mafanikio, changamoto, na hatua zinazochukuliwa katika utekelezaji wa Mradi wa HEET katika chuo hiki cha Mbeya, ili kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi na unaleta matokeo yaliyotarajiwa.
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi ilipokelewa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Mkoa wa Mbeya. Wajumbe walipata fursa ya kutembelea na kujionea miundombinu ya chuo na kupewa maelezo ya jumla kuhusu Chuo na utekelezaji wa mradi wa HEET.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Aloys Mvuma uliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa HEET, ikiwemo mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, changamoto zilizojitokeza, na mikakati iliyopo ya kuzitatua.
Taarifa ilijikita zaidi katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, na maendeleo ya kitaaluma kwa wahadhiri na wanafunzi. Kabla ya wasilisho hilo, Kamati ilitembelea maeneo ya ujenzi yanayofadhiliwa na mradi wa HEET, ikiwemo jingo la taaluma, maabara, madarasa, kituo cha ubunifu na uboreshaji wa ubunifu wa kibiashara.
Wajumbe walijionea maendeleo ya ujenzi na ubora wa vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunza.
Wajumbe wa Kamati walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa mradi wa HEET. Maswali mengi yalijikita katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za mradi, pamoja na mkakati wa kudumu wa kuboresha ubora wa elimu inayotolewa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Mwanasha Khamis Juma, Mwakilishi wa jimbo la Dimani, alieleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa mradi wa HEET. Alipongeza juhudi za uongozi na watendaji wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia kwa kufanikisha miradi mbalimbali licha ya changamoto zilizopo na kuipongeza SUZA kwa hatua iliyofikia na kuitaka iendelee kupata uzoefu ili kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji. Mwenyekiti alizitaka taasisi zote zinazohusika kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa ufanisi na kwa wakati unaotarajiwa. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka mikakati endelevu ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza ili kuboresha zaidi utekelezaji wa mradi.
Nae Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Moh’d Makame Haji, alitoa maelezo kuhusu fursa ambazo SUZA inapata kujifunza kutoka kwa watekelezaji wa mradi wa HEET. Alieleza kuwa ushiriki wa SUZA katika mradi huu unatoa nafasi muhimu ya kujifunza mbinu bora za utekelezaji wa miradi mikubwa ya elimu, ikiwemo usimamizi wa fedha, ujenzi wa miundombinu, na ufundishaji wa kitaaluma. Aidha, Makamu Mkuu alibainisha kuwa mradi wa HEET una nafasi kubwa katika kuimarisha sekta ya elimu ya juu Zanzibar kwa kuongeza uwezo wa Chuo kuzalisha wahitimu wanaohitajika na soko la ajira.
Kupitia mradi huu, SUZA inaimarisha vifaa na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, na kutoa mafunzo kwa wahadhiri ili kuboresha ubora wa elimu. Hii inasaidia kuwaandaa wanafunzi kwa mahitaji ya soko la ajira, hivyo kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar. Makamu Mkuu alisisitiza kuwa ushirikiano na kujifunza kutoka kwa watekelezaji wa mradi ni muhimu katika kufanikisha malengo haya na kuboresha zaidi sekta ya elimu ya juu.
Kwa upande mwengine, Dkt. Everest Mtitu, Msaidizi Mratibu Mkuu Kitaifa, ambaye pia alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, alizungumzia umuhimu wa mradi wa HEET kwa taifa la Tanzania. Alisisitiza kuwa mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya elimu ya juu nchini Tanzania, kwani unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hivyo kuongeza ubora wa elimu inayotolewa.
Dkt. Mtitu pia alieleza umuhimu wa kuwa na ushirikiano katika kutekeleza mradi huu ili ukamilike kwa ufanisi. Alionya kuwa iwapo taasisi moja itashindwa kutekeleza majukumu yake, mradi mzima utaathirika na kuingia dosari. Hivyo, alisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano na ushirikiano baina ya taasisi zote zinazohusika ili kuhakikisha mafanikio ya mradi wa HEET kwa manufaa ya taifa zima.
Zaira hii pia ilitoa nafasi kwa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi kutembelea ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambapo walikaribishwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Beno Malisa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ambae alieleza kufurahishwa kwake na uwepo wa ziara hii ambayo inadhihirisha mapenzi makubwa yaliyopo baina ya pande mbili za Muungano. Alieleza kuwa ziara hii ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa kila upande, ili kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha ushirikiano.
Mkuu wa Mkoa aliahidi kuendelea kushirikiana na SUZA na taasisi nyingine za Zanzibar katika juhudi za kuboresha elimu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika kutoa shukurani za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Lela Mohammed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, alitoa pongezi kwa serikali zote mbili na kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dr. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada kubwa wanazochukua katika kuiletea maendeleo nchi yetu.
Alieleza kuwa mradi huu ni wa kitaifa na unahusisha pande zote mbili za Muungano, na mafanikio yake ni kuboresha sekta ya elimu na kuleta maendeleo.
Aidha, aliwataka wasimamizi wa mradi kuwa makini na kuongeza nguvu katika usimamizi na kuhakikisha wale wote waliopata fursa za kusoma kupitia mradi huu wanamaliza kwa wakati na wanarudi kufanya kazi ili lengo la mradi lifanikiwe.
Kwa ujumla, ziara ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Mkoa wa Mbeya, ilikuwa na mafanikio makubwa. Kamati iliridhika na maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa HEET, pamoja na juhudi zinazofanywa na chuo katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Kamati inapendekeza kwamba juhudi zaidi zifanyike kushughulikia changamoto zilizobainishwa ili kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi na unaleta matokeo yanayotarajiwa. Aidha, imetoa wito kwa pande zote zinazohusika kuendelea kushirikiana na kuwekeza katika elimu ya juu kwa maendeleo endelevu ya Tanzania