The State University Of Zanzibar

SUZA, Kandarasi wasaini mkataba ujenzi wa Chuo

CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Kampuni ya Ujenzi ya Mohammed Builders Limited zimetiliana saini mkataba wa ujenzi wa majengo mawili ya Skuli ya Kilimo na Maabara unasimamiwa na Mpangosi.


Tukio hilo lililofanyika tarehe (4/11/2024) katika ofisi za Makao makuu ya SUZA Kampasi ya Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, limewashirikisha Makamu Mkuu wa SUZA na Kandarasi wa Kampuni ya Mohammed Builders Bw. Nizar Lakhani kutoka Dar es Salaam.

Ujenzi huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni na unatarajiwa kufanyika kwa muda wa miezi 18 ambapo utagharimu shilingi Bilioni 20.


Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi, Makamu Mkuu wa SUZA Prof. Haji alisema SUZa inatekeleza kazi inayoweza kuchangia maendeleo ya watakao kuwa nguvu kazi ya Taifa.


Alisema kuwa hii ni sehemu ya utekelezaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi katika elimu ya juu.


Aliongeza kuwa hatua hii imekuja kufuatia utafiti maalum uliofanywa na Serikali uliobaini upungufu mkubwa wa wahitimu hali iliyosababisha kupatikana mkopo wa Dola za Marekani Milioni 20 ambazo zimegawanywa katika maeneo tafauti ya utekelezaji wa mradi.

‘’Mradi huu unawekeza katika elimu ili kuleta mabadiliko makubwa katika uimarishaji miundombinu, mitaala na uwezeshaji wa wahitimu katika ngazi za uzamili na azamivu na kuangalia eneo la muhimu matumizi ya TEHAMA kwa kuweka mifumo ya teknolojia ya kisasa’’, alisisitiza Makamo Mkuu wa SUZA.


Aidha alisistiza kuwa utekelezaji wa kazi hiyo uende sambamba na kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi ya vijana kwani ujenzi huo hautanufaisha SUZA pekee lakini pia vijana wengi wanaotafuta elimu ya kujenza maisha yao na Taifa kwa jumla.


Alionya kuwa haitapendeza kutokea bahati mbaya jambo litakalozuia kutekelezeka mikataba ambayo pande hizi mbili zimetiliana saini huku tunamshirikisha Mshauri Elekezi katika kazi hii.


‘’Tusiiangushe Serikali, viongozi, na wananchi wanaoiamini Serikali yao kuwa itawatendea vyema, jukumu hili ni letu sote kwani utekelezaji huu unakwenda sambamba na Ilani ya Uchaguzi 2025’’, alitoa wito kwa wakandarasi, mshauri elekezi na jamii ya SUZA walioshuhudia utiaji wa saini.


‘’Serikali imetoa ahadi ya kuleta amabadiliko ya sekta ya elimu na sisi ni watekelezaji’’


Aliongeza kuwa hivi karibuni SUZA imezindua mradi mwengine wa ujenzi ambao nao majengo makubwa yatajengwa.


Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa kampuni ya Mohammed Builders Ltd Bw. Lakhani aliahidi kutekeleza kazi zao kwa umakini na ufanisi mkubwa kwani wana uzoefu katika kazi za ujenzi.


‘’Tumejiandaa, hata tukikabidhiwa leo kesho tunaanza kazi kwa ufanisi mkubwa’’, alisema kwa kujiamini.


Naye Mshauri Elekezi wa ujenzi huu, Bw. Lazaro Peter kutoka Kampuni ya Arqes Africa Ttd. aliwakumbusha wakandrasi kuwa na kauli thabiti ya utekelezaji wa mradi huo kwani Zanzibar hajawahi kushuhudia mkandarasi kufeli.


‘’Tusijikwae hatua ya kwanza wakati tuna safari ya miezi 1000, tukisema kesho ni kesho ’’, alisema Mshauri.