The State University Of Zanzibar

SUZA yapata mtaalamu elimu ya michezo

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimepokea mtaalamu atakayefundisha elimu ya sayansi ya michezo kwa ajili ya kuimarisha sekta hiyo katika Chuo hicho.


Akizungumza na mtaalamu huyo, Yutaka Ide anatokea Hiroshima nchini Japani, mazungumzo yaliyofanyika makao makuu ya SUZA Tunguu mkoa wa Kusini Unguja, Makamo Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Moh’d Makame Haji alisema amefarijika sana kuona sekta hiyo inaimarika kwa kuwa na wataalamu wa ndani na nje.

‘’Kutokana na uhusiano mzuri baina ya SUZA na Japan kupitia Shirika la JICA wametupatia mtaalamu wa kujitolea ambaye atatufudisha elimu kwa michezo na sayansi ya michezo kwani hatuna wataalamu wa kutosha’’, alisema Prof. Haji.


‘’Karibuni tutajenga viwanja vyenye huduma na vifaa vyote vya michezo tunavyohitaji kama vile kuogelea gym na nyengine’’, alisema.


Prof. aliahidi kuwa mipango ya kukamilisha taratibu itamazilika muda mfupi ujao ili aanze kazi ya kufundisha elimu kwa michezo na sayansi ya michezo. Katika kikao hicho ambacho kilimshirikisha pia mtaalamu wa ndani wa fani ya michezo, Prof. alisema kuwa anaamini kuwa kila upande utajifunza zaidi katika masuala ya michezo.


Aliongeza kuwa hivi sasa SUZA inatumia eneo dogo la Skuli ya Elimu kwa sababu hakuna vifaa vya kutosha isipokuwa vifaa vyengine vinatumiwa kutoka kwenye taasisi nyengine.


Aidha, Prof. alifurahishwa na mtaalamu huyo kuwa anaweza kuzungumza Kiswahili na kumshauri ajiunge na taasisi ya SUZA inayofundisha lugha kikiwemo Kiswahili kwa wageni.


Naye Yutaka alisema anakipenda Kiswahili, anafurahia kujifunza na kwamba anatenga muda kwa ajili ya kujifunza lugha hii kila siku.

Naye mkuu wa Skuli ya Elimu, Dk. Said Khamis ambaye alifuatana na mgeni huyo alisema wana matarajio kuwa malengo yaliyowekwa ya kuimarishwa sekta ya michezo kupatikana muda mfupi ujao.