Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Leila Muhammed Mussa, amesemateknolojia ya kisasa itaongeza kasi ya upatikanaji wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalum nchini.
Hayo aliyasema katika ufunguzi wa semina ya siku tatu iliyoanza leo tarehe 09/09/20024 katika Kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) huko Maruhubi. Katika semina hiyo ya Kuondoa Vikwazo vya Elimu: Urekebishaji Mbinu Jumuishi na Teknolojia katika Elimu Zanzibar alisema njia hii ya kisasa itabadilisha namna watu wenye ulemavu wanavyoweza kujipatia elimu kwa wepesi na kutatua changamoto zinazowakabili.
‘’Nimeridhishwa na kuona teknolojia inatumika katika ufundishaji kwa wanafunzi wenye ulemavu… tunaweza pia kuondosha pengo la upatikanaji wa elimu kwa kuimarisha utoaji wa elimu, na walimu kubuni mazingira ya ufundidhaji,’’ alisema.
Aliongeza katika kuweka mazingira bora kwa watu wenye ulemavu, Serikali italazimika kubadilisha mtaala wa elimu ili kubadilisha mbinu za ufundishaji, kuwa na miundombinu mahususi na kubadilisha mitazamo kwa wazazi kutambua namna ya kuishi na watu wenye mahitaji maalum.
Aidha, aliongeza kuwa mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika yanapaswa kuwahusisha watu wote wakiwemo wanafunzi, walimu na wazazi kutambua namna gani waishi na watu wenye ulemavu.
Alifahamisha kuwa hakuna uwiano kati ya wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na masomo katika ngazi za msingi na sekondari ikilinganishwa na vyuo vikuu.
‘’Wanafunzi wenye ulemavu wanaojiunga vyuo vikuu ni wachache mno ikilinganishwa na waliosajiliwa wanapoanza masomo, kila wakiendelea mbele wanapungua’’, alisisitiza.
Mapema, Makamo Mkuu wa SUZA, Prof. Mohd Makame Haji alisema kuwa mchango wa wadau wa maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha maendeleo ya elimu yanayotakiwa Zanzibar.
Alisema kuwa maendeleo ya sera ya Elimu ya Zanzibar yanayolenga kuondoa vikwazo vya Elimu ni ushuhuda wa utekelezaji wa jukumu hili.
Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi Theresa Zitting akizungumza kwa njia ya mtandao alisema wana matarajio makubwa kwa mradi huu kutatua changamoto za kielimu kwa watu wenye mahitaji maalum.
Aidha, alikiri kiwango cha elimu kwa watu wenye mahitaji maalum kiwamgo cha elimu kwa watu wenye ulemavu kiko chini hali inayochangiwa na kuwepo skuli chache kwa watu wenye wahitaji maalum na watoto kutopelekwa skuli.
Mafunzo hayo yanawashirikisha wadau mbali mbali wakiwemo kutoka taasisi zinazotoa mafunzo ya elimu mjumuisho, vyuo vya ualimu vya kati na mabaraza ya watu wenye ulemavu, yameandaliwa kwa ushirikiano baina ya SUZA na Chuo Kikuu cha Jamk cha Finland na kuwashirikisha pia wanachama walio kwenye mradi huo wakiwemo Chuo Kikuu cha Ruanda na Chuo Kikuu cha Tempere cha Finland