The State University Of Zanzibar

Dk. Hussein ahimiza kufanywa tafiti

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mhe. Dk. Hussein Mwinyi ametoa wito kwa jamii ya SUZA kutilia mkazo zaidi katika masuala ya kufanya tafiti kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi. Hayo aliyasema katika hafla ya uzinduzi wa Kigoda cha Taaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika makao makuu ya SUZA huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, alisema matokeo ya tafiti hizo yatatoa taarifa sahihi kwa watunga sera ili kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

Aidha, aliongeza kuwa huchangia pia kutambuliwa changamoto na fursa zilizopo katika sekta mbali mbai na watumiaji wa tafiti hizo wakiwemo wadau wa maendeleo na pia Serikali. Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kufanya tafiti na kazi nyengine za kitaaluma kupitia Kigoda cha Karume ili kustawisha taaluma na kuleta mchango katika jamii.

‘’Mtakapofanya hivyo mtakuwa mmekitendea haki Kigoda hiki na kumuenzi kwa vitendo Mzee wetu Marehemu Abeid Amani Karume’’, alisisitiza Dr. Mwinyi.

Kigoda cha Taaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume kina malengo mbalimbali yakiwemo; kuhifadhi, kuenzi na kuendeleza fikra za Sheikh Abeid Amani Karume katika kuleta ukombozi na maendeleo ya Zanzibar, kufanya SUZA kuwa ni mahali pa majadiliano, kuendeleza ushirikiano mwema ndani na nje ya Afrika, kukuza uwezo wa vijana na wasomi wanaochipukia kwa kuwashirikisha katika tafiti, makongamano, mikutano na mijadala ya Kigoda.


Naye Balozi wa Kigoda hicho, Dk. Amani Abeid Karume ambaye ni Rais wa awamu ya sita wa Zanzibar, alipongeza hatua hii na kueleza kuwa kuanzishwa kwa Kigoda ni kufungua ukurasa mpya wa historia kwani hii itakuwa ni chachu ya ukombozi na maendeleo ya nchi. Aliwataka vijana kuenzi mawazo na fikra za muasisi huyo kupitia nyaraka muhimu ili ziweze kuwasaidia lakini pia kuwa wadadisi kwa watu waliowazidi umri.
“Piteni na waulizeni hao asilimia sita (6) ya watu waliobakia ambao walizaliwa kabla ya Mapinduzi ya 1964, watakwambieni wanajua mambo ambayo nyinyi hamyajui’’, alikumbusha.

Alisema kuanzishwa kwa Kigoda hicho ni lazima viongozi wahakikishe wanasimamia na kuendeleza aliyoyaamini kiongozi huyo. “Ni lazima viongozi waenzi fikra za Mapinduzi kwa kudumisha umoja pamoja na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo kutoa elimu kwa usawa bila ya kuangalia sura, rangi au eneo la kijiografia kwani haya ndio malengo ya Mapinduzi yaliyoongozwa na Marehemu Karume na wenzake, kwa hivyo ni lazima yaendelezwe katika kufanikisha lengo la kuanzishwa kwa Kigoda”, alitoa msisitizo.
Katika kumkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Prof. Moh’d Makame Haji, alisema lengo la kuanzishwa kwa Kigoda hicho ni kuhifadhi, kuenzi na kuendeleza mawazo na fikra za Sheikh Abeid Amani Karume katika kuleta ukombozi na maendeleo.

Alisema Kigoda kitaandaa mijadala itakayolenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto kwenye nyanja za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisayansi ili kuzidi kuifanya SUZA kuendeleza azma yake ya kuwa ni kichocheo cha mabadaliko ya jamii.

Nae Mwenyekiti mteule wa Kigoda, Profesa Eginald Mihanjo alisema kuna kazi kubwa ya kuwajengea hamasa vijana kwani hawajui ukoloni, wala hawajui uhuru. Aliongeza kuwa hoja nyingi zinazozungumzwa na vijana hazina uzalendo, hazikuzi mapinduzi wala hazikuzi uchumi,’’ alisisitiza.

“Ni vyema kuangalia mikakati na operesheni na mbinu za Mzee Karume na kuzitumia ili kuona namna gani tunaweza kujenga nchi kwa kutumia falsafa zake’’, alisema. Katika kuchangia mjadala, SUZA iliwaalika watu mashuhuri miongoni mwao ni Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa awamu ya saba wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein Pamoja na mwanasiasa nguli Bwana
Stephen Wasira.

Kwa kuanza mjadala wa kuchangia mada, Dk. Kikwete alisema Kigoda ni kitu cha heshima kinacholenga kuendeleza tafiti na taaluma. Alisema SUZA imekuja na uamuzi sahihi kwa kuaznisha Kigoda hiki ambacho kitajikita katika ukombozi na maendeleo ya Afrika.

Aliendelea kueleza kuwa Vigoda hutoa hursa ya kuboresha na kuchochea maendeleo ya fani maalum huku vikitoa fursa ya kukuza ya kukuza ushirikiano na kuimarisha sera ya umataifishaji wa vyuo vikuu. Alishangazwa na hulka iliyopo ya vyuo vikuu katika zama hizi kukosa mchanganyiko wa wanataaluma maprofesa kutoka mataifa mbalimbali tofauti na ilivyokuwa zamani wakati wao wanasoma.

Kuhusu suala la utafiti alisema maendeleo yoyote duniani yanachangiwa na utafiti, ingawa sio utafiti tu unahitaji mipango lakini pia unahitaji gharama kwani ndio msingi wa maendeleo ya ufanyikaji wake. Alitoa rai kwa SUZA katika siku za baadae kuzalisha vigoda vingine akitolea mfano kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kina kigoda zaidi ya kimoja huku akivitaja vingine kuwa ni Kigoda cha Maendeleo ya Nyerere, Kigoda cha Mazingira, Kigoda cha Taaluma ya Kiswahili, Kigoda cha Bioteknolojia ambavyo alisema vyote vimeonesha mafanikio makubwa.

Nae Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake alisema Kigoda kina kazi kubwa ya kuyatunza Mapinduzi na kudumisha Muungano. Kigoda kina jukumu kubwa la kuendeleza mambo hayo, aliendelea kufahamisha hadhira.

“Ni lazima kuyakumbuka Mapinduzi na ni haki na wajibu kufanya hivyo ili kusambaratisha ubaguzi uliopingwa na viongozi walioasisi chini ya uongozi wa jemadari wake, Sheikh Karume”, alisema.

Dk. Shein aliendelea kueleza kuwa marehemu Sheikh Karume alikuwa na moyo wa ushujaa na uzalendo; alifanya mengi yaliyowanufaisha wananchi wa Zanzibar yakiwemo utoaji wa elimu bila malipo ambapo hata baada ya yeye kuuwawa na wapinga Mapinduzi viongozi wote waliofuatia walifuata nyao zake kwa kutoa elimu na afya bila ya malipo ikiwa ni uendelezaji wa falsafa zake.

Dk. Shein nae pia hakusita kuzungumzia suala la utafiti ambapo yeye alisema ni lazima ufanyike utafiti utakaochambua mustakbali wa taifa kwa kuoanisha na dira, fikra na muono wa marehemu Sheikh Karume.

Alisisitiza kuwa ni vyema kwa Kigoda hicho kuzingatia haiba ya marehemu Sheikh Karume ili kisije kikaliwa na mchwa baadae kwani mchwa bado wapo hivyo hiki kigoda kina jukumu la kuenzi na kufanya yale yaliyotaka kufanywa na kiongozi huyu shupavu, hivyo ni lazima sana sote tuwe tayari kukilea.

Mwanasiasa mkongwe Bwana Stephen Wasira yeye aliitumia fursa hii kwa kueleza kwa urefu historia ya Zanzibar katika mrengo wa kupatikana kwa ukombozi wake ambapo alisema Zanzibar ilikuwa imegubikwa na ubaguzi ambao hatimaye Marehemu Karume alipigana nao kuhakikisha anaondoa matabaka yaliyokuwepo.