Chuo Cha Taifa Cha Utalii (NCT), imetia saini hati ya makubaliano ya mashirikiano kati yake na Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar lengo likiwa ni kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kitaaluma katika fani za utalii na ukarimu.
Hati hiyo ya makubaliano imekuja baada ya kuona juhudi kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais Dkt . Hussein Mwinyi katika kuhamasisha na kutangaza sekta ya utalii kupitia Filamu ya Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo Cha Taifa Cha Utalii, Dkt. Florian Mtey amesema NCT na SUZA zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya taaluma kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa utalii.
“Tanzania ina vivutio vingi ambapo juhudi kubwa zimeendelea kufanyikana Marais wetu wawili katika kutangaza utalii na fursa za uwekezaji za Tanzania. Hivyo sisi kama wanataaluma tukaona tuendelee kuunga juhudi zao na kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ya utalii na ukarimu kwa viwango vya kimataifa amesema Dkt. Mtey .
Aidha Dkt Mtey alisema kwamba Vyuo hivyo vimekubaliana kuwa na program maalum ya kubadilishana wanataaluma na wanafunzi kati ya taasisi hizo.
Dkt. Mtey alisema pia kuwa Vyuo hivyo vitafanya mashirikiano kwenye maeneo mengine ikiwemo kutafuta maeneo ya kufanya mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya wanafunzi wa taasisi hizo na kuandaa mashindano mbalimbali kwenye fani ya upishi ambapo tayari NCT na Taasisi ya Utalii ya Zanzibar zimekwisha kufanya hivyo.
Aidha Dkt. Mtey amesema wao kama Chuo Cha Taifa Cha Utalii kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Taifa cha Zanzibar zitashirikiana kuandaa Tamasha la Chakula ambalo italenga kutangaza aina zote za vyakula vya asili vya Tanzania Bara na Visiwani.
“Hii yote ni kutaka kutangaza vivutio vyetu vya utalii kupitia Utalii wa kiutamaduni kupitia Tamasha hilo, amesema Dkt. Mtey.
Mbali na hayo Dkt. Mtey amesema kupitia mashirikiano hayo wanaandaa kongamano kubwa la kimataifa litakalofanyika tarehe 21-22 Novemba mwaka huu jijini Arusha, hivyo aliikaribisha Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Utalii Zanzibar kushiriki na kutoa mada mbalimbali kuhusu uchumi wa Buluu.
Kwa upande wake, Makamu wa Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar -SUZA , Profesa Mohamed Haji Makame amesema kuwa Tanzania Bara na Zanzibar zimeona jitihada nyingi zimefanyika katika kuimarisha Sekta ya utalii, hivyo watahakikisha Sekta ya utalii inaingia kwenye mpango mkakati wa Serikali na kuiwekea Sera maalumu ili kuimarisha uchumi .
“Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekuja na sera ya uchumi wa Buluu ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu zinazosimamia sera hiyo ni Sekta ya Utalii, mchango mkubwa unaotolewa unailetea Taifa letu pato na fedha za kigeni, lakini pia kusaidia jamii kubwa ya kitanzania kuweza kupata fursa mbalimbali zinazotokana na shughuli za utalii kwa kupata ajira na kufanya shughuli ambazo zinawapatia kipato. Sekta hii nayo imewekwa katika mpango maalumu” amesema Prof. Haji.
Ameongeza kuwa uchumi wa Buluu kwa upande wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni eneo ambalo linaimarika kwa kasi, na hiyo inatokana na juhudi za Serikali zetu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Taasisi zetu za taaluma zinajikuta ziko nyuma kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na juhudi za Serikali zetu katika kuendeleza mbele maendeleo ya sekta ya utalii.Hili limetufanya tukae kwa pamoja ili kujitathmini na kuangalia mikakati iliyobora ya kuongeza nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuboresha Sekta ya utalii.