Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA YAFANYA KIKAO CHA 10 KUFUATILIA MAENDELEO YA UJENZI WA DAHALIA ZA WANAFUNZI NA MKAHAWA

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kupitia Kamati inayosimamia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa dahalia za wanafunzi na mkahawa, kimefanya kikao cha 10 pamoja na Mkandarasi kutoka Kampuni ya M/S Emirates na Mshauri Elekezi kwa ajili ya kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 27 Septemba 2026 katika eneo la ujenzi wa mradi huo, Makao Makuu ya SUZA, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupitia na kutathmini hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, pamoja na kujadili masuala yanayohusiana na maendeleo ya kazi za ujenzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo ya mradi, ujenzi wa dahalia ya wanafunzi umefikia asilimia 33, huku ujenzi wa dahalia ya wanaume pamoja na mkahawa ukiwa umefikia asilimia 15.

Mradi huo unalenga kuongeza na kuboresha miundombinu ya huduma kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, hususan katika maeneo ya malazi na huduma za chakula.

Kikao hicho cha 10 kinaonesha umuhimu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kuzingatia mipango, viwango vinavyohitajika na malengo yaliyowekwa na Chuo.

SUZA inaendelea na juhudi za kuimarisha miundombinu ya Chuo kwa lengo la kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kuishi kwa wanafunzi wake.